OBARA: Miundomsingi mijini izingatie uboreshaji afya ya wakazi
Na VALENTINE OBARA
SIKU ya Majiji Ulimwenguni iliadhimishwa Alhamisi iliyopita bila shamrashamra nyingi, ambapo suala lililopewa kipaumbele na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lilihusu hali ya afya kwa wanaoishi mijini.
Ulimwenguni kote, ripoti huonyesha kwamba wakazi wa mijini hasa miji mikuu hukumbwa na matatizo mengi ya kiafya yanayoweza kuepukika.
Magonjwa yanayoshuhudiwa sana miongoni mwa wakazi wa miji mikuu ikiwemo Nairobi huwa yanaweza kuzuiwa sana sana kupitia kwa ulaji wa lishe bora na muhimu zaidi, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara.
Changamoto lililopo ni kwamba wakazi wengi hukosa muda wa kufanya mazoezi ikizingatiwa mahitaji ya kujitafutia riziki usiku na mchana.
Ni kwa msingi huu ambapo WHO inapendekeza viongozi watilie maanani hitaji la kujenga miundomsingi inayoweza kusaidia wakazi kufanya mazoezi ya mwili wanapoendelea na shughuli zao za kawaida za kila siku.
Katika baadhi ya mataifa yaliyoendelea kiuchumi, miundo ya miji hutoa kipaumbele kwa ujenzi wa miundomsingi inayorahisisha usafiri kwa baiskeli au matembezi.
Kwa bahati mbaya, miji ya Kenya ikiwemo Nairobi hujali tu jinsi ya kupanua barabara kwa njia sambamba na ongezeko la magari ya kibinafsi kila kukicha. Hii ni licha ya kuwa imebainika wazi kupitia utafiti kwamba upanuzi wa barabara mijini hauwezi kutatua misongamano ya magari.
Kwa sasa, uendeshaji baiskeli mijini kama mbinu ya uchukuzi ni balaa tupu! Unapowazia kung’ang’ania barabara moja na matatu zinazoendeshwa na madereva wakorofi, utaona ni sawa na kujitakia maafa ya mapema.
Vilevile, kutembea pia ni tatizo jingine kwani miji yetu haina sehemu mwafaka zilizo safi na salama za kutembelea kutoka mitaani hadi katikati ya mji. Hakika, hata kutembea kutoka baadhi ya vituo vya magari ya umma hadi sehemu za kazi ni shida.
Serikali za Kaunti zinaweza kuleta manufaa mara mbili iwapo zitatilia maanani umuhimu wa kujenga miundomsingi ya uendeshaji baiskeli na kutembea.
Kwanza, mbinu hizi za uchukuzi zitatoa nafasi kwa umma kufanya mazoezi ya mwili kila siku wanapoenda kazini, hivyo basi kupunguza maradhi kama vile ya moyo.
Pili, wengi hawatahitaji kutumia magari na hivyo basi muda wanaopoteza katika misongamano barabarani itatumiwa kwa majukumu mengine yanayoweza kuimarisha uchumi wa miji na nchi kwa jumla.
Viongozi mijini wana jukumu kubwa linaloweza kuchangia katika afya bora ya wananchi hata wanaporahisisha uchukuzi wa umma.