Ukahaba ni hatia kama uavyaji mimba – Serikali
Na GEOFFREY ONDIEKI
SERIKALI imeapa kumaliza shughuli za ukahaba mjini Nakuru ambazo zimekithiri mitaani.
Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Bw Erastus Mbui aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa kuna mipango ya kumaliza uovu huo.
Makahaba wanajishughulisha na uovu huo wameripotiwa kuwalazimisha wanaume wanaotumia mitaa hiyo kuchangia kwa utovu wa salama.
Bw Mbui alitaja shughuli hizo za ukahaba zinazoendelea mitaani kuwa kinyume na sheria za Kenya. “Hakuna kibali cha ukahaba nchini Kenya. Ni hatia, kama vile ushoga na uavyaji mimba,” alisema.
Kamishna huyo aliongeza kuwa watashirikiana na serikali ya kaunti kuhakikisha uovu huo unaondolewa.
“Tumepata habari kuwa kundi hilo la mwanawake wana muungano na unaongozwa na kiongozi wao, tutabaini nani aliwasajili na kuwapa kibali,” alisema Bw Mbui.
Hata hivyo, alikiri kutopata malalamishi kutoka kwa polisi kuhusu madai ya wanaume kusumbuliwa wakitumia mitaa hiyo. “Naomba wale wanaume ambao wamesumbuliwa kivyovyote vile wapige ripoti kwa polisi ili watusaidie kuwakamata wahusika,” alisema.
Shughuli za ukahaba hufanyika katikati mwa mji wa Nakuru, Kanu street, Maeneo ya ThreeWays na mtaa wa Kiambuthia.
Wakati mwingine huwa vigumu kwa wapita njia hasa wanaume kutumia mitaa hiyo wakiwa na wake wao kwa sababu [makahaba] huwalazimisha wanaume kwenye mitaa hiyo.
Taifa Leo ilipotembea maeneo ya Kisii Road, Kanu Street na maeneo ya Threeways, ilithibitisha ukweli wa madai haya.
Mwendo wa saa nne asubuhi, kina dada wa umri tofauti wanaonekana wameegema kuta wakiwa wamevalia nusu uchi.
Mmoja wao ambaye aliomba jina lake lisitajwe alisema kuwa wanawake wengi hufanya biashara hii ya ukahaba kutokana na umaskini na changamoto za kimaisha.
“Inatubidi kufanya hii kazi kukidhi mahitaji ya familia zetu na sio eti tunapenda anasa kama wengi wanavyofikiri,” alisema.
Bi Jane [sio jina lake halisi] aliongeza kuwa wasichana wengi wa vyuo vikuu wanajiingiza kwenye biashara hii chafu kwa tamaa ya kupata pesa kirahisi na mwishowe wanakuwa waraibu.