Makala

SEKTA YA ELIMU: Undumakuwili huu wa TSC utakuja kuiponza yenyewe

November 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHARLES WASONGA

MPANGO wa Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) kufutilia mbali uhusiano wake na Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) ambao umedumu kwa zaidi ya miaka 50 utafifisha ushawishi wa chama hicho kama mshirika mkuu katika sekta ya elimu.

Hii ni kwa msingi wa umuhimu wa chama hicho sio tu kama mtetezi wa masilahi ya walimu bali pia masuala yanayohusiana na mchango wake katika utayarishaji wa sera za elimu.

Afisa mmoja wa cheo cha juu katika wizara alikuwa na haya ya kusema kuhusu Knut: “Kimsingi, chama ni cha umuhimu mkubwa kwetu kwa sababu kinatupa jukwaa la kufanya mazungumzo na walimu sio kuhusu masuala ya masilahi pekee, bali katika masuala ya sera. Kwa hivyo, ikiwa TSC itakosa kuitambua (Knut) wakati huu ambapo chama kinazongozwa na mvutano wa uongozi, kitapoteza nguvu yake kama chombo cha kutetea masihali ya walimu na kuchangia sera ya elimu.”

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia alitoa ilani Jumatatu; ya miezi miwili kwa Knut, kuwa inapanga kuvunja mkataba wa kukitambua chama hicho kama chama rasmi cha walimu.

Dkt Macharia anasema Knut haina idadi hitajika, kisheria, ya wanachama ambao wameajiriwa na TSC na hivyo haiwezi kutambulia kama chama cha walimu.

Afisa huyo anasema kulinga na Sheria za Leba, sharti chama cha walimu kiwe na asilimia 50 na moja ya walimu wote walioajiriwa na TSC ndiposa kitambuliwe rasmi.

Kulingana na tume hiyo, sajili ya TSC ina jumla ya walimu 318,000 ambao wameajiriwa katika shule za msingi na upili za umma na hivyo “Knut inapaswa kuwa na angalau wanachama 159,000.

Lakini tume hiyo inasema kuwa Knut, ambacho ni mojawapo ya vyama kongwe vya wafanyakazi nchini, kufikia sasa kina wanachama 115,ooo pekee katika sajili yake.

Hata hivyo, ajabu ni kwamba TSC haikutoa idadi ya walimu wa vyuo vya kadri katika sajili yake, wengi wao wakiwa wanachama wa chama cha kutetea masilahi ya walimu za shule za upili (KUPPET).

Tangazo la Dkt Macharia limejiri siku chacha baada ya TSC kuondoa jina la Katibu Mkuu wa Knut Wilson Sossion katika orodha ya walimu nchini na hivyo kumzima kufunza katika shule yoyote ya umma na upili. Tume hiyo ilichukua hatua hiyo kutokana na hali kwamba Sossion ni mbunge maalum wa ODM.

Lakini ni kinaya kwamba TSC inapania kukatiza mkataba wake na Knut kwa sababu wanachama wake hawajatimu asilimia 50 na moja ya walimu wote iliyoajiri ilhali haijatoa ilani kama hiyo kwa Kuppet ambayo pia haijatimiza hitaji hilo.

Hii ni kwa sababu wakati huu, chama cha Kuppet kilichoanzishwa mnamo 1998, kina wanachama 120,000 pekee walioajiriwa na TSC.

Idadi hii ilipanda kutoka 80,000 mnamo Agosti 2019 baada ya zaidi ya wanachama 20,000 wa Knut kukigura.

Hii ni baada ya TSC kusitisha nyongeza ya mishahara ya wanachama wa Knut kufuatia agizo la mahakama.

Mahakama ilikataa pendekezo la TSC kwamba awamu hiyo ya tatu ya nyongeza ya mishahara ya walimu itolewe kwa misingi gredi ya walimu wala sio vyeo wanavyoshikilia.

Hatua hiyo ilikuwa pigo kwa walimu wakuu, manaibu wao na walimu waliohudumu kwa miaka mingi, hali iliyowafanya kugura Knut, iliyowasilisha kesi hiyo mahakamani, na kujiunga na Kuppet.

Isitoshe, tangu mwaka jana, TSC imekuwa ikihujumu Knut kwa kudinda kuwasilisha michango ya kila mwezi ya wanachama wake ili kuilemeza kifedha.

Na katika mzozo wa uongozi katika chama hicho, TSC iliegemea mrengo unaoongozwa na Naibu Katibu Mkuu Hesbon Otieno ambao Agosti ulitangaza kumng’oa mamlakani Bw Sossion.

Na kinaya kingine ni kwamba TSC inamzima katibu huyo mkuu Knut kwa misingi ya kuwa mbunge, ilhali inawasaza maafisa wa Kuppet ambao pia ni wabunge.

Wao ni mwenyekiti Omboko Milemba ambaye ni Mbunge wa Emuhaya (ANC), Catherine Wambilianga (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa kaunti ya Bungoma) ambaye ni katibu wa Kuppet katika Kaunti ya Bungoma na Ronald Tonui (Naibu Mwekahazina wa Kitaifa) ambaye ni mbunge wa Bomet ya Kati (Jubilee).