• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wahuni wa Sonko wapiga waandishi

Wahuni wa Sonko wapiga waandishi

Na BENSON MATHEKA

KUNDI la wanaume walioandamana na Gavana wa Nairobi, Mike Sonko Jumanne lilitatiza utulivu katikati ya jiji walipozua vurugu wakijaribu kuzuia wanahabari kunasa picha zake akienda kuhojiwa kwa udanganyifu.

Katika machafuko hayo, Bw Sonko na wanaume hao waliwashambulia wanahabari waliokuwa wakifuatilia akipelekwa katika ofisi za Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Katika kizaazaa kilichozuka nje ya ofisi za EACC, Bw Sonko alirekodiwa akimshambulia mpigapicha wa gazeti la Standard, Bw Collins Kweyu.

Mwanamume mwingine aliyekuwa nyuma ya Bw Sonko pia alimpiga mwanahabari huyo.

Kwenye taarifa, Baraza la Wanahabari (MCK) lilisema wanahabari wengine pia walishambuliwa kwenye kizaazaa cha jana.

Wanahabari hao ni Steve Shitira (Citizen TV), Jeff Angote (Nation) na Joseph Wakhungu (Milele Fm).

Afisa Mkuu Mtendaji wa baraza hilo, David Omwoyo alisema baraza liliona kanda ambayo Bw Sonko alirekodiwa akimshambulia Bw Kweyu.

“Tunataka kuwakumbusha waliotekeleza uovu huu kwamba uhuru wa wanahabari ni haki iliyotambuliwa katika katiba, na jaribio lolote la kuwazuia wanahabari kutekeleza kazi yao ni ukiukaji wa katiba,” alisema.

Bw Sonko alikuwa ameitwa na maafisa wa EACC kuhojiwa kuhusu madai kwamba alitoa habari za uongo kwa tume kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Jana, wafuasi wake waliandamana hadi afisa za tume hata kabla yake kuwasili na ikabidi polisi wafyatue hewa ya kutoa machozi kuwatawanya. Kizaazaa kilizuka polisi walipomzuia Bw Sonko kuingia katika lango kuu la ofisi hizo kwa gari lake.

Ni alipopishwa kuingia langoni ambapo aliinua mkono na kumchapa kofi Bw Kweyu aliyekuwa akijiandaa kumpiga picha.

Bw Omwoyo alihimiza maafisa wa usalama kuheshimu uhuru wa wanahabari wakiwa kazini.

You can share this post!

SEKTA YA ELIMU: Undumakuwili huu wa TSC utakuja kuiponza...

IEBC yajitetea kuhusu sajili ya wapigakura Kibra

adminleo