Wapigakura eneo la Kibra waanza kutekeleza haki yao kidemokrasia
Na COLLINS OMULO na SAMMY WAWERU
WAKAZI wa Kibra, Kaunti ya Nairobi na ambao ni wapigakura wameanza kutekeleza haki yao ya kidemokrasia leo Alhamisi asubuhi na mapema kuchagua mbunge katika uchaguzi mdogo hii ikiwa ni baada ya kifo cha Ken Okoth kilichotokea Julai baada ya kuugua saratani kwa muda.
Vituo vimefunguliwa saa kumi na mbili asubuhi ambapo foleni ndefu zinashuhudiwa katika wadi tano za eneobunge hilo ambazo ni Sarang’ombe, Woodley/Kenyatta Golf Course, Makina, Laini Saba, na Lindi.
Kuna jumla ya wagombea 24 wanaowania kiti hicho. Idadi ya wapigakura ni 118,658.
Chama cha ODM alichotumia Okoth wakati wa uhai wake sasa kimemdhamini nduguye ambaye ni Bernard Imran Okoth, nacho chama tawala cha Jubilee kimemdhamini McDonald Mariga.
Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna amesema kila kitu kilikuwa kikiendelea vizuri huku akielezea matumaini kwa mgombea wao.
“Kufikia sasa hakuna tukio lolote la kuhujumu mchakato huu,” amesema Sifuna.
Kiongozi wa ODM Raila Odinga amekuwa mstari wa mbele kipindi chote cha kampeni kumpigia debe Imran Okoth huku Naibu Rais William Ruto akimpigia debe mwanasoka Mariga.
Wagombea wengine ni Eliud Owalo wa Amani National Congress (ANC) na Khamisi Butichi wa Ford-Kenya.
Kabla ya Jumapili, muda rasmi rasmi uliowekwa na tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) harakati za kampeni kufikia kikomo, viongozi wa vyama shirika walijitokeza na kupigia debe wawaniaji wao.
Kiongozi wa ODM Raila Odinga, alivutia na anaendelea kuvutia ngoma upande wa Imran, akidai Kibra ni ngome ya ODM. Mariga, akionekana kuleta ushindani mkali, Naibu wa Rais Dkt William Ruto amefanya ziara kadhaa eneo hilo, kumfanyia kampeni mwanasoka huyo.
Sawa na viongozi hao, Musalia Mudavadi wa ANC na Seneta Moses Wetangula wa Ford – Kenya, wamekuwa katika mstari wa mbele kutetea wawaniaji wao.
Ni kinyang’anyiro ambacho kimeonekana kuleta mgawanyiko katika chama tawala cha Jubilee, baadhi ya viongozi wake wakiongozwa na mbunge maalum Maina Kamanda na gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi Kamotho, wakijitokeza hadharani kuunga mkono mgombea wa ODM.
Ingawa hatua hiyo inakosolewa na baadhi ya wandani wa Dkt Ruto, inaonekana kama kuimarika kwa demokrasia. Wajuzi wa masuala ya kisiasa wanasema mkondo wa aina hiyo ukiigwa katika siku za usoni, hususan wakati wa uchaguzi mkuu, utaonesha ukomavu wa demokrasia Kenya.
“Si jambo la kawaida chama pinzani kuungwa mkono na kile tawala. Viongozi wanapaswa kuchaguliwa kulingana na rekodi ya utendakazi. Hilo linaonesha ukomavu wa demokrasia,” asema Dan Machuki.
Hatua ya Imran kupigwa jeki na baadhi ya viongozi wa Jubilee kuibuka mshindi, Naibu Rais anaitafsiri ‘Odinga kuomba msaada’ kwa kuwa ‘kitanda chake’ eneobunge la Kibra alipohudumu kama mbunge kwa muda mrefu linataka kukombolewa.
Mjadala huo pia umezua mdahalo mkali mitandaoni, wanablogu na wachangiaji wakieleza hisia na mtazamo wao.
Uchaguzi huo unachukuliwa kama njia ya Dkt Ruto kupimana nguvu na Bw Raila, katika kurithi siasa za kaunti ya Nairobi.
Shughuli ya uchaguzi huo mdogo zikiendelea, idadi ya watu waliojitokeza kushiriki inasemekana kuwa ya chini mno.
Kiongozi wa ODM Raila Odinga tayari amepiga kura yake, akihimiza wakazi wa Kibra kujitokeza kwa wingi.
“Watu waruhusiwe kuonesha haki yao kidemokrasia kwa kushiriki uchaguzi huu mdogo bila kushawishiwa na yeyote. Tuko katika kitanda chetu, na ninasihi watu wajitokeze kwa wingi,” Waziri huyo Mkuu wa zamani akasema, akionekana kulenga madai kuwa kuna uhongaji wa wapigakura.
“Watu wanaotoa pesa na wengine kupokea, uhongaji, huo ni ufisadi na haionyeshi demokrasia,” akaeleza Bw Odinga.
Kwa mujibu wa sajili ya IEBC, eneobunge la Kibra lina jumla ya wapigakura 118,658. Lina jumla ya vituo 183 vya kupiga kura.
Vituo vitafungwa saa kumi na moja za jioni, kisha shughuli za kuhesabu kura zing’oe nanga na kutumwa katika kituo maalum cha shughuli hiyo.
Kulingana na IEBC, matokeo hayatapeperushwa kieletroniki kama ilivyoshuhudiwa 2013 na 2017.