TAHARIRI: Sonko ameupaka tope uongozi nchini
NA MHARIRI
HATUA ya Gavana Mike Sonko wa Nairobi kutumia wafuasi wake kuzua rabsha mnamo Jumanne katika makao makuu ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inaibua maswali kuhusu uwajibikaji wa kiongozi huyo.
Bw Sonko alikuwa ameagizwa na tume hiyo kufika mbele yake kutoa ufafanuzi kuhusu maelezo aliyotoa ili kuruhusiwa kuwania ugavana mnamo 2017.
Hata hivyo, alijitetea vikali, akisema kuwa EACC haina mamlaka ya kumwagiza kutoa maelezo hayo, ikizingatiwa aliruhusiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwania ubunge mnamo 2010 na useneta mnamo 2013.
Ingawa kila mtu ana haki ya kujitetea dhidi ya madai anayokabiliwa nayo, anafaa kufanya hivyo kwa kufuata kanuni za kisheria zilizowekwa. Bila shaka, hatua ya Bw Sonko ilizua taswira mbaya, kwamba viongozi nchini wanaweza kukwepa sheria kwa kuwachochea wafuasi wao kuzua ghasia.
Kwa muda mrefu, imekuwa kawaida kwa viongozi nchini kutumia kila mbinu kukwepa adhabu licha ya uzito wa makosa ambayo huwakabili.
Hilo ndilo limetajwa kuwa kikwazo kwa maafisa wanaoshiriki katika kashfa za ufisadi kuchukuliwa hatua.
Kutokana na mtindo huo, viongozi hupora fedha za umma kimakusudi kwa kufahamu kuwa hakuna adhabu yoyote watachukuliwa.
Hilo ndilo limetuzalia sakata kama Goldenberg, Anglo-Leasing, Triton, Eurobond, kati ya zingine ambapo mabilioni ya pesa za umma yamepotea bila waliohusika kuwajibika hata kidogo.
Katika sakata ya Goldenberg, vikao vya wazi kuchunguza waliohusika havikuzaa matunda yoyote kwa Wakenya licha ya serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki kutumia mamilioni ya pesa kuwalipa majaji na mawakili walioshiriki.
Mtindo uo huo ndio umedhihirika chini ya utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, ambapo washukiwa wakuu wa sakata mbalimbali huwa wanafikishwa mahakamani bila hatua zozote kuchukuliwa baada ya hapo.
Kwa mfano, hakuna mshukiwa hata mmoja mwenye ushawishi ambaye amehukumiwa kutokana na kupotea kwa zaidi ya Sh1.8 bilioni katika Shirika la Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS).
Hivyo, kitendo cha Sonko kinatia doa mfumo mzima wa uongozi nchini.