• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Walinzi 4 wa sonko washtakiwa kwa kutusi polisi

Walinzi 4 wa sonko washtakiwa kwa kutusi polisi

Na Richard Munguti

WALINZI wanne wa Gavana Mike Sonko walikamatwa tena Jumatano baada ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh100,000 na mahakama ya Nairobi.

Haikubainika sababu ya kuwatia nguvuni tena kwa washtakiwa hao. Mmoja wa walioshtakiwa jana alikuwa amevalia nguo zilizoraruriwa.

Walinzi hao John Abok, Joseph Mwangi Kirai, Kennedy Odhiambo na Richard Bosire walikamatwa wakitoka seli baada ya kulipiwa dhamana na Bw Sonko.

Wanne hao walikabiliwa na mashtaka matatu ya kuwazuia maafisa wa polisi wakiwatia nguvuni, kushiriki katika mkutano usio halali na kuzua vurugu.

Washtakiwa hao walikanusha kwamba, mnamo Novemba 5, 2019 mwendo wa saa tano asubuhi, katika makao makuu ya tume ya kupambana na ufisadi (EACC) walikataa wakitiwa nguvuni na maafisa watano wa polisi.

Washtakiwa hao walidaiwa kukataa kukamatwa na maafisa wanne wa Polisi Konstebo Peter Mwangi, Timothy Nyagah, Silas Soita, Joseph Muturi na Antony Kasili.

Shtaka lilisema maafisa hao wa polisi walikuwa kazini washukiwa hao walipokataa wakishikwa. Shtaka la pili lilisema kuwa washtakiwa hao wakishirikiana na wengine ambao hawakufikishwa kortini walishiriki katika mkutano usio halali katika jengo la Integrity iliyoko mtaa wa Upper Hill kaunti ya Nairobi.

Shtaka lingine dhidi yao ni kuzua vurugu na kuhatarisha amani. Kiongozi wa mashtaka alimweleza hakimu mwandamizi Mahakama ya Milimani Bw Kennedy Cheruiyot kwamba washtakiwa hao walisababisha vurugu kwa kuwatukana maafusa wa kulinda usalama kwa kuwaita wajinga.

Shtaka lilisema wanne hao waliwatukana polisi kwa kusema , “ninyi wajinga tupigeni risasi.”

Hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot aliwaachiliwa washtakiwa kwa dhamana ya Sh100,000 na kuwaamuru wawasilishe pasipoti zao mahakamani.

You can share this post!

Vijana 3,000 washukiwa wa magenge wakamatwa

Jiandae kwa mvua kubwa mwezi huu

adminleo