Imran Okoth ashinda kiti cha ubunge Kibra
Na CECIL ODONGO
MWANIAJI wa Chama cha ODM katika uchaguzi mdogo wa Kibra Imran Bernard Okoth ndiye atakakuwa mbunge mpya wa Kibra mara atakapoapishwa, hii ni baada ya ushindi wake kuthibitishwa Ijumaa asubuhi.
Hii ni baada ya Imran kumbwaga mgombea wa Jubilee McDonald Mariga na wagombea wengine kwa kuzoa kura 24,636 baada ya kujumuishwa matokeo ya vituo vyote 183.
Bw Mariga amepata kura 11,230 zilizohesabiwa na kukubalika.
Bw Eliud Owalo ambaye aliwania kwa tiketi ya ANC alipata kura 5,275 huku Khamisi Butichi wa Ford Kenya akifunga orodha ya nne-bora kwa kupata kura 260 pekee.
Idadi jumla ya wagombea ilikuwa ni 24.
Afisa msimamizi wa IEBC eneobunge la Kibra Bi Beatrice Muli ametangaza matokeo rasmi katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo cha City Inspectorate Dagoretti.
“Ningependa kumtangaza Imran Okoth kama mbunge mteule wa Kibra baada ya kushinda uchaguzi mdogo wa Kibra. Shukrani kwa wawaniaji wote kwa kushirikiana vizuri kuhakikisha uchaguzi huu unafanikiwa,” amesema Bi Muli.
Imran sasa atarithi kiti hicho kilichosalia wazi baada ya kifo cha nduguye, marehemu Ken Okoth aliyeaga dunia kutokana na ugonjwa wa saratani mnamo Julai 2019.
“Ninawashukuru sana wapigakura wa Kibra kwa kunipigia kura na kuonyesha kwamba pesa haziwezi kununua uongozi. Namshukuru sana kiongozi wa chama chetu Raila Odinga na viongozi wote wa ‘handisheki’ walionifanyia kampeni. Naomba wapinzani wangu tushirikiane kujenga Kibra,” amesema Imran.
Kutangazwa kwa Imran mshindi Ijumaa – siku moja baada ya uchaguzi wenyewe – kumepokelewa kwa shangwe na vigelegele na wabunge wa ODM na baadhi ya wale wa Jubilee waliomuunga mkono.
Uchaguzi huo ambao ulitajwa kama vita vya ubabe wa kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa upinzani Raila Odinga sasa unafungua ukurasa mpya wa kisiasa, wabunge waliosifia ushindi wa Imran wakiahidi kuanzisha kampeni ya kuvumisha Jopo la Maridhiano (BBI).
Ripoti ya BBI inatarajiwa kuwasilishwa kwa Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta.
Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed amesema pamoja na viongozi wengine wataendelea kuwahimiza Wakenya kuishi kwa mshikamano mzuri.
“Wakenya sasa wanajitambua na hawataki kugawanywa na wanasiasa wasiojielewa,” amesema Mohamed.
Eneobunge la Kibra lina idadi ya wapigakura 118,658 waliosajiliwa.
Ni asilimia 35.35 waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi mdogo uliofanyika Alhamisi.
Kura 41,984 zilikubalika huku 259 zikipuuzwa kwa sababu kadhaa.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa Jubilee walisema matokeo ya uchaguzi huo yanaonyesha kwamba Dkt Ruto anaendelea kupata umaarufu Kibra na mwaniaji wa Jubilee huenda akashinda kiti hicho mwaka 2022 jinsi ilivyofanya katika eneobunge jirani la Langata mwaka 2017.