Habari Mseto

Cotu kusukuma kuteuliwa kwa mkuu wa NSSF

November 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

MUUNGANO wa kitaifa wa vyama vya wafanyakazi Kenya (COTU-K) umetishia kwenda mahakamani kusukuma kuteuliwa kwa Afisa Mkuu katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii na Mafao (NSSF).

Kulingana na katibu wa Cotu Bw Francis Atwoli, juhudi za kumteua msimamizi zimekuwa zikigonga mwamba na kupingwa na baadhi ya watu wenye maslahi binafsi.

Afisa mkuu wa sasa na baadhi ya wakurugenzi wakuu katika shirika hilo wako katika nafasi za ukaimu.

“Haya ni baadhi ya maswala ambayo yanachangia katika kuzembea kwa utendakazi katika shirika hilo. Cotu itaenda mahakamani kusukuma hatua ya kuchaguliwa kwa msimamizi haraka iwezekanavyo,” alisema Bw Atwoli katika taarifa.

Atwoli alipeana mfano wa hivi punde ambapo bodi ya NSSF ilifanya mkutano ambao ulihudhuriwa na wanachama wa muungano wa Cotu ambapo Bw Anthony Omerikwa aliibuka mshindi katika uteuzi.

Alimlaumu mwenyekiti wa bodi Jenerali (Mstaafu) Dkt Julius Karangi na Waziri wa Leba Ukur Yatani kwa kutotilia maanani suala hilo linalowaathiri mamilioni ya wafanyakazi.

Msimamizi anapoteuliwa, mwenyekiti wa bodi huwasilisha jina lake kwa Waziri wa Leba kwa uchunguzi unaohusu msasa.

Bw Atwoli alisema kuwa licha ya kuandika barua kwa Dkt Karangi kuhusu swala hilo miezi miwili iliyopita, hawajapokea jibu lolote.

“Kutokana na kimya cha wawili hao, Cotu inajiandaa kuelekea mahakamani juma lijalo,” aliongeza.

Nafasi hiyo ya kazi ilichapishwa mnamo Aprili 2019.