Machar na Kiir wana siku zingine 100 kuunda utawala wa mseto
Na MASHIRIKA
ENTEBBE, UGANDA
RAIS wa Sudan Kusini Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar wamekubaliana kuahirisha kuunda serikali ya muungano kwa siku 100 baada ya kukosa kusuluhisha tofauti zilizozuka, hatua iliyosababisha Amerika kuonya kuwa nchi hiyo inayokumbwa na mzozo pengine itakuwa bora zaidi ikiwapata viongozi wapya.
Mahasimu hao wawili ambao tofauti zao zilisababisha mzozo na vifo vya maelfu ya raia, waliruhusiwa kuahirisha kuunda serikali ya kugawana mamlaka baada ya kukutana ana kwa ana nchini Uganda.
Hii ilikuwa mara ya pili viongozi hao kuahirisha makataa tangu muafaka waliofikia Septemba kusitisha vita. Pande zote zilikuwa zimekubaliana kushirikiana katika serikali ya muungano wa kitaifa kufikia Novemba 12.
Lakini tarehe hiyo ilikaribia huku masuala kadhaa yakiwa bado hayajatatuliwa na viongozi wa eneo wakawaita Entebbe kuyajadili.
“Haikuwa rahisi kwao kukubaliana katika muda wa siku tano. Tumewapatia miezi mitatu na tutaendelea kufuatilia,” alisema waziri wa mashauri ya kigeni wa Uganda baada ya viongozi hao kukutana faraghani katika ikulu ya Entebbe.
“Walikubaliana kuahirisha muda wa kuanza kipindi cha mpito na kuchunguza hali baada ya siku 50 kuanzia siku hiyo,” Kutesa alisema akisoma taarifa rasmi ambayo viongozi hao walitoa pamoja.
Amerika, inayounga nchi hiyo ilitamaushwa na hatua hiyo na ikasema itachunguza upya uhusiano wake na serikali ya Sudan Kusini.
“Kukosa kuafikia makataa yao wenyewe kunazua maswali kuhusu uwezo na ufaafu wao wa kuendelea kuongoza mchakato wa amani katika nchi hiyo,” alisema Tibor Nagy, balozi wa Amerika kuhusu Afrika akirejelea Kiir na Machar.
“Amerika inachunguza njia zote inazoweza kutumia kushinikiza watu hao wanaokwaza amani na kusababisha machafuko,” aliandika kwenye ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter.
Amerika imekuwa ikitisha kuwekea vikwazo viongozi wa Sudan Kusini ingawa afisa mmoja aliondoa hofu nchi hiyo itasitisha msaada wa kibinadamu kwa nchi hiyo wa kiasi cha cha Sh1 trilioni.
Nagy aliwasifu wapatanishi wa Afrika wakiwemo marais Yoweri Museveni, Abdel Fattah al-Burhan anayeongoza baraza la mpito Sudan na Kalonzo Musyoka, balozi wa Kenya anayehusika na mzozo wa Sudan Kusini.
Baadhi ya wadadisi wanasema kusukuma pande zote kuunda serikali ya mpito kabla ya kuzika tofauti zao kabisa hasa kuhusu mipaka kunatishia kurejesha nchi hiyo katika vita.
Mkataba wa amani umerejesha utulivu katika nchi hiyo vita vilipozuka miaka miwili baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka Sudan.
Watu zaidi ya 400,000 waliuawa na milioni nne kufurushwa makwao. “Ni heri waahirishe kwa mara nyingine badala ya vita kuzuka tena,” alisema Alan Boswell, mdadisi wa shirika la International Crisis Group.