• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Sababu ya KRA kuwaandama washukiwa wa ukwepaji ushuru

Sababu ya KRA kuwaandama washukiwa wa ukwepaji ushuru

Na CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) imeimarisha juhudi zake za kupambana na wafanyabiashara wanaokwepa ushuru kwa sababu Wizara ya Fedha imeiwekea kiwango cha juu cha ushuru inaofaa kukusanya mwaka huu wa kifedha.

Katika mwaka huu wa kifedha, 2019/2020, KRA inahitajika kukusanya jumla ya Sh1.8 trilioni kama ushuru kutoka humu nchini ili kufadhili bajeti ya kitaifa ya Sh3.02 trilioni iliyosomwa Juni 2019.

Itakumbukwa kuwa katika mwaka wa kifedha wa 2018/2019 KRA ilihitajika kukusanya Sh1.6 trilioni kama ushuru kutoka humu nchini lakini ikamudu Sh1.4 trilioni pekee.

Kwa hivyo, kutokana na presha ya kutaka kukusanya ushuru zaidi KRA imeamua kuwafikisha mahakamani wakurugenzi wa kampuni mbalimbali ikiwashtaki kukwepa kulipa mabilioni ya fedha kama malimbikizi ya ushuru.

Kwa mfano, mnamo Agosti 2019 wakurugenzi wa kampuni ya kutengeneza pombe na mvinyo ya Keroche Breweries Limited Tabitha Karanja na mumewe Joseph Karanja walikamatwa kwa madai ya kukwepa kulipa ushuru wa kiasi cha Sh14.5 bilioni.

Hatua kama hiyo ilichukuliwa dhidi ya mmiliki wa kampuni ya African Spirit Limited Humprey Kariuki kwa tuhuma za kukwepa kulipa malimbikizi ya ushuru yanayofikia Sh41 bilioni.

Mbinu hii inayotumiwa na KRA katika kuwaandama wakwepaji ushuru imevutia hisia za wafanyabiashara wengi; baadhi wakidai ni dhalimu na inakwenda kinyume na sheria.

Wengine wameitaka KRA kubuni njia mbadala na “za kiutu na kistaarabu” za kuhakikisha kuwa kampuni mbalimbali na wafanyabiashara wanatimiza wajibu wao wa kulipa ushuru.

“Ni aibu kuona wawekezaji wa humu nchini ambao wameajiri vijana wetu wakiabisha kwa kusumwa korokoroni eti kwa sababu wamekosa kulipa ushuru. Nadhani kuna njia za kistaarabu ambazo KRA inaweza kutumia kushughulikia suala hili, badala ya kuwakamatwa wafanyabiashara na kuwafikisha kortini. KRA inapasa kuhimiza uwekezaji wala haipasi kuonekana kuwanja moyo watu kama hawa,” anasema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watumiaji Bidhaa (Cofek) Bw Stephen Mutoro.

Rais Uhuru Kenyatta vilevile, ametoa wito kwa KRA kuendeleza mikakati ambayo sio “dhalimu” zaidi inapaendeleza kampeni ya kuhakikiksha kuwa kampuni mbalimbali zimelipa ushuru inavyotakikana.

“Baadhi ya kampuni hizi hazijui kama zimetenda kosa. Kwa hivyo, muongee nao kwa sababu ni wateja wenu ili kufahamu wajibu wao,” akasema Rais Kenyatta alipoongoza hafla ya kuzituza kampuni zilizoongoza katika ulipaji ushuru mwaka 2018.

Hafla hiyo iliandaliwa katikati mwa wiki.

You can share this post!

Bweni lateketea tena shuleni Musingu

SANAA: Talanta yake yamfaa pakubwa maishani mnamo wakati...

adminleo