• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
IDAH MUNGIRIA: Mwigizaji wa Auntie Boss anavyofuata nyayo za Anna Kendrick

IDAH MUNGIRIA: Mwigizaji wa Auntie Boss anavyofuata nyayo za Anna Kendrick

Na JOHN KIMWERE

‘MTAKA cha mvunguni sharti ainame.’ Ndivyo wahenga walivyolonga na tangu zama zile ndivyo hali ilivyo hadi sasa.

Ni msemo ambao umeonekana kuwa na mashiko kwa kiwango fulani miongoni mwa jamii.

Pia unaonekana unaendelea kudhihirishwa na kina dada wengi tu ambao wameamua kujituma mithili ya mchwa kwenye masuala tofauti katika harakati za kusaka riziki.

Miongoni mwao ni binti, Idah Mwendwa Mungiria mwana maigizo anayeibukia, mwana mtindo chipukizi pia mwanafunzi wa mwaka wa pili kwenye Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN ). Dada huyu anasomea kuhitimu kwa shahada ya digrii katika masuala ya biashara za kimataifa.

Alianza kujituma katika masuala ya uigizaji miaka miwili iliyopita alipojiunga na kundi la Imara Arts, pia kipindi hicho alikuwa akisomea masuala ya maigizo chini ya kundi la Nairobi Performing Arts Production.

”Nilitamani kuwa mwana maigizo tangu nikiwa mdogo maana mara nyingi nikiwa na marafiki zangu tulikuwa tukishiriki mchezo wa kuigiza nyumbani,” alisema na kuongeza kuwa tokeo kipindi hicho ndipo alijiwekea azma hiyo.

Hata hivyo, alipata motisha zaidi alipotazama kipindi cha ‘Tahidi High’ mwaka 2009 ambacho hupeperushwa kupitia Citizen TV.

”Nilipendezwa na uigizaji wake Sarah Hassan aliyejulikana kama Tanya katika kipindi hicho pia nilivutiwa na ushiriki wake, Catherine Kamau aliyefahamika kama Selina katika kipindi cha Mother inlaw.” Kipindi hicho pia hupeperushwa kupitia Citizen TV.

Anasema wakati huo alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne kwenye shule ya St Marys Ruaraka, Nairobi.

Dada huyu anasema anataka kushiriki maigizo akilenga kufikia kiwango chake mwigizaji mahiri mzawa wa Marekani, Anna Cooke Kendrick aliyeshiriki filamu iitwayo ‘Pitch Perfect’ iliyovuma mwaka 1985. Picha/ John Kimwere

Kisupa huyu anajivunia kushiriki filamu kadhaa zilizopata mpenyo kupeperushwa kupitia runinga tofauti ikiwamo ‘Auntie Boss’ (NTV), ‘Varshita’ ‘Selina’ na ‘Njoro wa Uba’ zote Maisha Magic East.

Ingawa hajapata mashiko katika uigizaji maana ndio mwanzo, ameanza kupiga ngoma, na anasema ana imani tosha atapiga hatua ndani ya miaka kadhaa ijayo.

Mrembo huyu anajivunia kufanya kazi na makundi mbali mbali tangu aanze kujihusisha na masuala ya uigizaji ikiwamo Badilisha Arts Production na Moonbeam Production kati ya zingine.

Ili kujiongezea maarifa anatamani sana kushirikiana na waigizaji wa kigeni hasa Jackie Appiah (Ghana) aliyeigiza filamu kama ‘Beyonce:The Presidents Daughter,’ na ‘The King is Mine.’

Pia Fulu Mugovhani (Afrika Kusini) aliyeshiriki filamu ya ‘Ayanda’ na ‘Lion King’ kati ya zinginezo.

Kisura huyu anawaponda Wakenya ambao hupenda kupuuza filamu za Wazalendo na kuwanyima nafasi ya kusonga mbele.

Anasema Wakenya wanastahili kuwa mstari wa kwanza kuziunga mkono kazi za wenzao kinyume na mtindo wao ambapo wanapenda kutazama filamu za kigeni.

Licha ya kuwa hajakomaa katika uigizaji sio mchoyo wa mawaidha, anahimiza wanadada wanaoibukia kujipa moyo na kujiamini wanaweza.

You can share this post!

Kalonzo aelekea kwa Ruto?

BELINDA ODHIAMBO: Usikubali kuvunjwa moyo na visiki katika...

adminleo