Hasara unga wa Dola kupigwa marufuku
NA MISHI GONGO
Ziadi ya malori 40 ya mahindi kutoka nchi ya Uganda na Tanzania yameegeshwa nje ya lango la ghala la kampuni ya kutengeza unga ya Kitui Flour Mills mjini Mombasa, madereva lake wasijue la kufanya baada ya kampuni hiyo kutakiwa kusitisha shughli zake na Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa, KEBS hapo Jumamosi.
Kulingana na wakazi wa eneo la Majengo lililo karibu na kampuni hiyo ya kusaga unga wa Dola, malori hayo yamekuwa katika eneo hilo kwa muda wa wiki mbili sasa yakisubiri kupakiwa bidhaa hiyo..
Kampuni hiyo ni miongoni mwa nne nyengine ambazo bidhaa zake za unga wa mahindi ulipatikana ukiwa na viwango vya juu vya sumu aina ya aflatoxin.
Aina zingine za unga ni Kifaru kutoka kampuni ya Alpha Grain Limited, Starehe unaotengenezwa na kampuni ya Pan African Grain Millers, 210 kutoka kampuni ya Kenblest na Jembe kutoka Kensal Rise Limited.
Baadhi ya wauzaji walilazimika kuuza unga huo kwa bei ya kutupa siku ya Jumamosi ili kumaliza shehena ambazo walikuwa wamenunua.
Unga wa mahindi kilo mbili wa Dola uliuzwa kwa Sh50 katika maeneo ya Bombolulu, Jomvu na Mishomoroni mjini Mombasa, licha ya kupigwa marufuku.
Siku ya Jumapili baadhi ya maduka ya jumla na maduka ya rejareja bado yalikuwa yanauza unga huo.
Wakaazi katika mji huo waliiomba serikali kuchunguza vyakula vinavyouzwa nchini kwa makini kabla ya kuviruhusu kusambazwa sokoni kwa matumizi.
“Kutoa ripoti ya kuonya watu baada ya unga kusambazwa sokoni inaonyesha serikali kuwa inazembea, kuna watu ambao wameshatumia unga huo,”alisema Bw Ali Hashim Mkazi wa Bombolulu.
Mwengine, Bw Rahim Aziz alitaka serikali kufuatilia mitambo inayosaga mahindi kuhakikisha shughuli hiyo inafanyika katika mazingira salama.
“Mara nyengine tunanunua unga tunakuta una madonge, na hata kuwa na ladha ya uchachu. Hii husababisha watu kuumwa na tumbo na hata kuharisha hivyo tunataka serikali kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa sokoni ni salama kwa binadamu,”alisema Bw Aziz.
Aliongezea kuwa watakaoshindwa kufikia viwango vya ubora wa bidhaa basi serikali inafaa kufunga kampuni zao.
Bi Miriam Jaffar alisema hajaona matatizo yoyote na unga alioununua wiki iliyopita.
“Mimi hununua vitu kwa jumla,sasa siwezi mwaga unga nusu bandali kwa kuhofia sumu ambayo haijanidhuru,nimekula unga huu na sijapatwa na matatizo yoyote,” alisema.
Ripoti iliyotolewa na kampuni ya unga ya Kitui Flour Mills ilisema walishtushwa na ripoti ya Kebs kuwa bidhaa zao zina viwango vya juu vya sumu aina ya aflatoxin wakisema kuwa madai hayo hayakuwa ya kweli.
Ilijitetea kuwa kwa zaidi ya miaka 20 wamekuwa wakitengeza bidhaa zenye ubora wa hali ya juu kwa wateja wao.
Shirika la Kebs lilisema lilifikia uamuzi huo baada ya kufanya uchunguzi na kupata malalamishi kutoka kwa Wakenya.
Limeonya wafanyabiashara dhidi ya kununua unga kutoka kampuni hizo nne. Atakaeyepatikana na bidhaa hizo zitachukuliwa na kuharibiwa pasi na malipo.