Serikali, dini zapinga mada za ushoga katika kongamano
GEORGE SAYAGIE, CECIL ODONGO NA SHABAN MAKOKHA
NAIBU Rais Dkt William Ruto jana alipinga hoja yoyote kujadiliwa kuhusu ushoga kwenye Kongamano la Kimataifa Kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo (ICPD) ambalo linatarajiwa kuanza rasmi kesho jijini Nairobi.
“Hatutakubali mada yoyote ambayo inakinzana na tamaduni na imani yetu ya kidini ijadiliwe kwenye kongamano hilo,” akasema Dkt Ruto akiwa katika Kaunti ya Narok.
Rais Uhuru Kenyatta pia aliwaonya wanaoandaa kongamano hilo la kimataifa kwamba Kenya haiko tayari kukumbatia tabia ambazo zinaenda kinyume na tamaduni yake na maadili.
Viongozi wa Kiislamu walionya waumini wao dhidi ya kulihudhuria kongamano hilo wakisema yatakayojadiliwa au kuzungumziwa hayaendani na maadili ya Kiafrika na dini yao.
Kulingana na Mwenyekiti wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu (CIPK) Abdallah Ateka, masuala ambayo yatajadiliwa kwenye kongamano hilo la siku tatu yanakinzana na mafundisho kwenye kitabu takatifu cha Koran.
Mnamo Ijumaa, Maaskofu wa Kanisa Katoliki waliwashutumu waratibu wa kongamano hilo kwa kulitumia kuvumisha ndoa ya jinsia moja kisha kuwashauri vijana kujihusisha na ngono za mapema ilhali mambo hayo mawili yamekataliwa kwenye dini na tamaduni za jamii ya Kiafrika.
Lakini mashirika ya kijamii kupitia mratibu wa shughuli zao Suba Churchill nayo yaliungana mkono kongamano hilo na kuonya viongozi wa kisiasa na wale wa kidini dhidi ya kulisambaratisha ilhali litakuwa linazungumzia namna ya kuheshimu haki za makundi mbalimbali ya raia.