Makabiliano mapya baina ya madiwani yatarajiwa Nairobi
NA COLLINS OMULO
MALUMBANO zaidi yanatarajiwa Jumatatu katika Kaunti ya Nairobi huku viongozi wapya walioidhinishwa kutwaa nyadhifa za Kiongozi wa Wengi na Kiranja wa Wengi wakitarajiwa kuingia afisini kuchukua nafasi za Abdi Guyo na Waithera Chege ambao walishikilia nafasi hizo awali lakini wakabanduliwa na wenzao wa chama cha Jubilee.
Huku viongozi wapya Charles Thuo ambaye ni diwani wa Dandora 3 na diwani maalum June Ndegwa waliopokezwa nafasi za wawili hao mtawalia wakiapa kuingia afisini, Bw Guyo na Bi Chege nao wameshikilia kwamba hawaendi popote wakisema sheria haikufuatwa wakati wa kuwatimua.
Diwani wa Ziwani Kariokor Millicent Mugadi naye aliteuliwa Naibu Kiongozi wa wengi kuchukua mahala pa mwenzake wa Riruta James Kiriba.
Spika Beatrice Elachi aliidhinisha mabadiliko haya ya uongozi ambayo sasa yanaashiria kwamba uongozi wa chama cha Jubilee kwenye bunge hilo hautasalia kama mwaka jana.
“Mabadiliko haya ni rasmi na yametekelezwa kwa kufuata Katiba kwa sababu tayari yamewasilishwa bungeni. Hata hivyo, kama kuna utata wowote basi wanachama wanafaa kufuatilia utata huo na uongozi wa chama,” akasema Bi Elachi.
Washikilizi hao watatu wa nyadhifa hizo mpya waliapa kuendeleza uongozi unaojumuisha viongozi wote huku wakiahidi kushirikiana na Bi Elachi kufanikisha utendakazi wa Bunge la Kaunti.
Hata hivyo, Bw Guyo amepinga mabadiliko hayo, akisema sheria haikufuatwa kumwondoa mamlakni kwa kuwa madiwani wote wa chama cha Jubilee bungeni humo hawakujumuishwa.
Vile vile, anadai kwamba Katibu wa Jubilee Raphael Tuju hakuandaa mkutano na madiwani wa chama hicho na kumwondoa afisini.
“Hizo njia mbili hazikufuatwa. Hakuna mkutano wa chama ulioitishwa na nitabanduka tu iwapo kiranja ataitisha uchaguzi na nishindwe kwa kupitia kura. Hata hivyo, wanajua kwamba nitashinda ndiyo maana wanatumia mlango wa nyuma kunibandua afisini,” akasema Bw Guyo.