Kimataifa

Upinzani Bolivia wazima vituo vya habari vya serikali

November 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA AFP

VIONGOZI wa upinzani nchini Bolivia Jumapili walivamia kituo cha runinga na kile cha redio, vyote vinavyomilikiwa na serikali na kuvikomesha kupeperusha matangazo hewani.

Hayo yalijiri huku uhasama wa kisiasa ukiendelea kutanda nchini humo.

Uhasama huo umechochewa na vuta ni kuvute kuhusu matokeo ya uchaguzi wa urais ambapo Rais wa sasa Evo Morales alitangazwa mshindi mwezi uliopita.

Waandamanaji ambao ni wafuasi wa kiongozi wa upinzani Carlos Mesa, ambaye pia aliwahi kuwa rais, walivamia runinga ya Bolivia TV na kituo cha redio ya Patria Nueva kueleza ghadhabu yao kwamba vituo hivyo vimekuwa vikiegemea upande wa Rais Morales.

Kulingana na mkurugenzi wa kituo cha redio cha Patria Nueva, Ivan Maldonado, waandamanaji hao waliwafurusha watangazaji hao na kuwaamrisha waondoke baada ya kupokeo jumbe za vitisho katika siku za nyuma.

Wafanyakazi zaidi ya 40 walionekana wakiondoka kwenye vituo hivyo huku waandamanaji waliokuwa nje wakiwamiminia kila aina ya matusi vituo hivyo vikiruhusiwa kucheza muziki pekee.

Tukio hilo lilikuwa kisa cha hivi punde kudhihirisha kero ya upinzani ambao unalalamikia udanganyifu kwenye uchaguzi huo uliompa Rais Morales nafasi ya kuongoza kwa muhula wa nne.

Rais Morales naye alishtumu kitendo cha uvamizi wa vituo hivyo, akisema wameonyesha kwamba hawaheshimu demokrasia.

“Wanasema wanapigania demokrasia lakini wanajifanya kwa kuwa vitendo vyao vinaonyesha udikteta. Pia wamevamia redio inayomilikiwa na Muungano wa wakulima,” akaandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mapema jana, Rais huyo alikuwa ametoa wito kwa viongozi wa upinzani wakubali kufanya mazungumzo naye ili waafikiane jinsi taifa hilo linaweza kusonga mbele na kumaliza visa vya utovu wa usalama vinavyotekelezwa na waandamanaji.

Hata hivyo, Mesa alikataa kuridhia ombi hilo akisema hawana chochote cha kuzungumza na Rais huyo wanayedai aliwaibia kura zao.

Uwezekano wa Rais huyo kuendelea kusalia mamlakani unaendelea kuwa finyu baada ya mgawanyiko kuanza kushuhudiwa kwenye vitengo vya polisi huku baadhi waliokuwa wakilinda afisi yake wakiondoka Jumamosi.

Ni maafisa wachache tu ndio walisalia kutoa ulinzi kwenye afisi hizo kufikia jana, ishara tosha kwamba hii huenda ikawa mwanzo wa kuporomoka kwa utawala wake.

Viongozi wa upinzani nao wametoa wito kwa jeshi la taifa hilo kufuata nyayo za polisi hao huku wakisisitiza kwamba uchaguzi huru ndio utatuliza mambo nchini humo.