Walowezi kufurushwa katika misitu 18 – Tobiko
Na GEORGE MUNENE
SERIKALI inapanga kuwafurusha watu wote wanaoishi kinyume cha sheria katika maeneo 18 yaliyotengwa na serikali kama chemchemi ya maji nchini.
Kulingana na Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko, wale ambao wameingilia maeneo hayo wanafaa kuanza kuondoka kabla ya wao kufurushwa.
Akiongea jana katika kijiji cha Rubora katika Kaunti ya Kirinyaga wakati wa shughuli ya upanzi wa miti, Bw Tobiko alionya kwamba mtu yeyote ambaye amejenga makao ndani ya msitu atafurushwa bila kujali mwegemeo wake wa kisiasa.
“Ninawaonya walowezi. Sharti waondoke ndani ya misitu wapende wasipende,” akasema.Bw Tobiko alikariri kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kuwa misitu yote inahifadhiwa na kwamba wanaoiharibu wanakabiliwa kisheria.
“Tumeondoa watu waliokuwa wakiishi ndani ya msitu wa Maasai Mau kinyume cha sharia. Na sasa tunapanga kuwaondoa watu kutoka misitu mingine. Hatutaruhusu watu fulani kuharibu misitu yetu na hivyo kuwaathiri Wakenya wengine,” akasema.
Bw Tobiko alisema serikali imejitolea kutimiza lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 10 ya nchi hii ni misitu kufikia 2022.
“Amri ya Rais sharti iheshimiwe na watu wanaoharibu misitu waondolewe. Tunalenga kupanda jumla ya miche milioni mbili,” akasema.
Bw Tobiko aliwataka wabunge kutoka Rift Valley kukoma kuingiza siasa katika shughuli ya kuwaondoa walowezi haramu katika msitu wa Mau.