Dawa feki zafurika madukani
Na LEONARD ONYANGO
HEWA chafu, maji yenye sumu na kufurika kwa dawa feki na zilizopitwa na wakati ni miongoni mwa hatari zaidi zinazowakumba Wakenya.
Kulingana na Wizara ya Mazingira, takribani Wakenya 14,300 hufariki kila mwaka kutokana na maradhi yanayosababishwa na hewa chafu.
Zaidi ya Wakenya milioni 7 wanaoishi katika miji mikuu nao wako katika hatari ya kuambukizwa maradhi wa kupumua hewa chafu kutoka kwa magari, viwandani, majiko na stovu.
Bodi ya Kudhibiti Dawa na Sumu (PPB) kwa ushirikiano na shirika la WHO, mapema Agosti, mwaka huu walitoa tahadhari kuhusu dawa feki ya kukabiliana na bakteria ambazo zimekuwa zikiuzwa nchini Kenya na Uganda.
Maafisa wa PPB walifanikiwa kunasa dawa hiyo ya Amoxicillin trihydrate – Potassium clavulanate katika baadhi ya maduka jijini Nairobi.
Kati ya 2016 na 2017, bodi ya PPB ilifunga maduka 670 yaliyoshukiwa kuuza dawa feki au zilizopitwa na wakati.
Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Forodha (WCO) iliyotolewa 2017 iliorodhesha jiji la Mombasa kuwa miongoni mwa bandari zinazoongoza barani Afrika kwa kuingizia bidhaa feki vya matibabu kutoka China na India hivyo kuhatarisha maisha ya mamilioni ya Wakenya.
Inakadiriwa kuwa watoto 250,000 hufariki dunia kila mwaka humu nchini baada ya kutumia dawa feki inayodaiwa kutibu malaria na homa ya mapafu (nimonia).
Ufisadi ndio unaolaumiwa kutokana na hatari hizi baada ya maafisa wa serikali kufumba macho.Maji machafuRipoti ya WHO ya 2019 inaonyesha kuwa ni asilimia 59 tu ya Wakenya wanaokunywa maji safi na salama.
Hiyo inamaanisha kuwa asilikuwa asilimia 41 ya Wakenya wanakunywa maji machafu na yasiyo salama hivyo kuhatarisha afya zao.
Kenya pia imeorodheshwa kati ya mataifa ambayo maji yake ya mfereji ni hatari kwa afya duniani.Repoti ya kampuni ya Globehunters ambayo husaidia watalii kuzuru nchi mbalimbali, ilisema kuwa maji ya mfereji nchini Kenya si salama na yanaweza kudhuru wageni.
Kulingana na Wizara ya Afya, watoto 89,000 hufariki kila mwaka humu nchini kutokana na maradhi yanayotokana na maji au mazingira machafu.Wakenya hutumia Sh27 bilioni kutibu maradhi yanayotokana na maji machafu.