• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Ruto apondwa na mawaziri kwa kumpuuza Rais

Ruto apondwa na mawaziri kwa kumpuuza Rais

Na NDUNGU GACHANE

MATAMSHI yaliyotolewa wikendi na baadhi ya mawaziri dhidi ya Naibu Rais William Ruto kuhusu anavyofanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta, yameashiria mgawanyiko katika baraza la mawaziri.

Vile vile, ishara imeonyesha Naibu Rais ametengwa katika upangaji shughuli za kiserikali.

Mawaziri watatu waliomwakilisha Rais katika harambee mjini Kenol, walitumia mafumbo kumshambulia Naibu Rais, wakimkashifu kwa mambo mengi kama vile kupinga handisheki ya Rais Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, kuzindua miradi ya serikali kanisani na kudharau agizo la Rais kutaka siasa za mapema zikomeshwe.

Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Bw Joe Mucheru, alianza kwa kusifu handisheki akisema ni muujiza uliowezesha serikali kuendeleza mipango yake.Alikosoa baadhi ya Wakenya kwamba wana macho na masikio ilhali hawataki kuona miujiza inayotokana na handisheki.

“Manufaa ya handisheki ni kwamba tumefanikiwa kupatia maendeleo kipaumbele na kufanikisha sensa ambayo haingewezekana bila handisheki,’ akasema.Matamshi hayo yalionekana kumlenga Dkt Ruto na wandani wake ambao hudai handisheki ni njama ya kumwezesha Bw Odinga kuingia mamlakani kwa njia haramu.

Waziri wa miundomsingi, Bw James Macharia alipohutubu, alisema Rais atazuru Murang’a kibinafsi kuzindua miradi ya maendeleo ili kuzuia baadhi ya watu kuizindua makanisani na kwingineko.Waziri huyo aliomba wakazi kuchagua uongozi ambao utaendeleza miradi iliyoanzishwa na Rais.

“Miradi tuliyoanzisha lazima ikamilike. Hili halitawezekana kama hatuna uongozi bora ndiposa tunapofanya mambo haya, tuhakikishe tutakabidhi mamlaka ya uongozi wa nchi hii kwa watu ambao watahakikisha hatua hizi zinaendelea,’ akasema.

Kwa upande wake, Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i alisisitiza kwamba mamlaka makubwa aliyopewa na Rais yalinuia kuhakikisha Rais Kenyatta anakamilisha malengo yake.

Alitumia mahubiri ya Askofu Julius Karanu kuhusu ufisadi, kuomba wenzake serikalini wajihadhari wanapotekeleza majukumu yao.

“Mahubiri yametufunza kutumikia nchi yetu kwa bidii, ukakamavu na uadilifu. Rais amejitolea kwa maendeleo na utoaji huduma pekee na jinsi Biblia inavyotufunza, kuna wakati wa kufanya kila jambo. Sasa ni wakati wa kufanya kazi. Tuungane na Rais, tumwombee anapotumikia nchi hii,’ akasema.

Kwingineko, Waziri wa Biashara na Viwanda, Bw Peter Munya alimkashifu Dkt Ruto kwa kupinga mipango ya serikali ikiwemo shughuli za jopo la maridhiano (BBI) akisema hakuna vile mtu anaweza kutangaza anafanya kazi na Rais ilhali mienendo yake ni kinyume na hilo.

“BBI ni mpango wa serikali kwa sababu jopo liliajiriwa na Rais kwa hivyo huwezi kusema uko pamoja na Rais ilhali unapinga mpango huu. Kila nafasi unayopata, unaitumia kwenda kinyume na mkubwa wako. Huwezi kuendelea kusema uko pamoja naye,’ akasema kwa mahojiano ya simu.

Hata hivyo, alisema shughuli za serikali hazijaathirika kwani Rais pekee ndiye ana mamlaka ya kuongoza mikutano ya baraza zima la mawaziri.

Rais asipokuwa nchini, Dkt Matiang’i husimamia mikutano ya kamati ya mawaziri kushauriana kuhusu masuala ya kiserikali.

You can share this post!

Dawa feki zafurika madukani

Polisi wageuka wanyama ghafla wakizima maandamano JKUAT

adminleo