• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 6:47 AM
Obado aomba korti imtimue wakili wa familia ya Sharon

Obado aomba korti imtimue wakili wa familia ya Sharon

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Migori, Bw Okoth Obado anayekabiliwa na shtaka la kumuua mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno ameomba mahakama kuu imtimue wakili anayewakilisha familia ya marehemu.

Bw Obado aliyeshtakiwa pamoja na aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na aliyekuwa mfanyakazi wa kaunti hiyo Casper Obiero ameeleza kuwa Prof George Wajackoya alikuwa mmoja wa mawakili wake na “ana ushahidi muhimu na taarifa za kisiri anazoamini zitatumika dhidi yake”.

Bw Obado amefichua kuwa jina la Prof Wajackoya halikujumuishwa miongoni mwa mawakili waliofika kortini Septemba 24, 2018 kumtetea.

“Prof Wajackoya aliudhika sana kwa jina lake kuondolewa. Alilalamika kwangu,” akasema Obado.Tangu wakati huo, aliteuliwa na familia ya Sharon kuiwakilisha.

Gavana Obado anaomba mahakama imzuie Prof Wajackoya kuwakilisha familia ya wahasiriwa akidai “Prof Wajackoya alikuwa mmoja wa mawakili wake kabla ya kubadili nia na kuanza kutetea familia hiyo ya wahasiriwa.

Mshtakiwa huyo anaomba mahakama imtimue Prof Wajackoya kwa kuwa atatumia habari zote alizomweleza dhidi yake.

Katika ombi hilo alilowasilisha mbele ya Jaji Jessie Lesiit Jumatano wiki iliyopita , Bw Obado alimedokeza kuwa punde tu alipokamatwa Septemba 23, 2019, Prof Wajackoya alimwendea katika kituo cha polisi alipokuwa amazeuliwa na kujitambulisha kwake.

“Siku mbili baada ya kukamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi, Prof Wajackoya alifika na kunieleza kuwa amekuwa akimfanyia kazi Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI),” Bw Obado alifichua katika taarifa ya kiapo (afidaviti) aliyowasilisha mahakamani.

Mshtakiwa alisema Prof Wajackoya alimwonyesha barua alizokuwa amewasiliana na DPP na DCI kuhusu masuala mbalimbali.

“Baada ya kunionyesha barua hizo, wasiwasi uliniondoka na bila shaka nikafahamu Prof Wajackoya ana ufahamu mkubwa katika masuala ya sheria. Nilimwagiza anitetee katika kesi hii ya mauaji,” Bw Obado alidokeza katika ombi la kuondolewa kwa wakili huyo (Wajackoya).

“Nilimweleza Prof Wajackoya kila kitu nilichofahamu kutuhusu mimi na Sharon. Kwa kuwa nilimwamini, nilimuuliza anitetee katika kesi hiyo ya mauaji,” asema Gavana Obado.

You can share this post!

Wazee wa Agikuyu sasa wapanga kusimamia tohara

Kalonzo ahusishwa na mauaji ya mtu katika mzozo wa ardhi

adminleo