• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
HAWASHIKIKI! Manchester City kama vile wameanza kukata tamaa

HAWASHIKIKI! Manchester City kama vile wameanza kukata tamaa

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, UINGEREZA

KOCHA Pep Guardiola amesema hana uhakika iwapo kikosi chake cha Manchester City kitaweza kuziba pengo la alama tisa ambalo kwa sasa linatamalaki kati yao na Liverpool ambao ni viongozi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Man-City wanalenga kuweka historia ya kuwa kikosi cha kwanza baada ya Manchester United kunyanyua mataji ya EPL kwa misimu mitatu mfululizo. Man-United waliufikia ufanisi huo mnamo 2009 chini ya aliyekuwa mkufunzi wao, Sir Alex Ferguson.

Kufikia sasa, Man-City waliopepetwa 3-1 na Liverpool wikendi iliyopita, wanashikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la ligi kwa alama 25, moja nyuma ya Leicester City na Chelsea.

“Siwezi kutabiri yajayo. Sijui chochote kitakachofanyika katika jumla ya mechi 26 zilizosalia msimu huu. Hata hivyo, nafahamu kuwa hakuna kisichowezekana katika ulingo wa soka,” akasema Guardiola kwa kusisitiza kuwa kubwa zaidi katika maazimio yao ya sasa ni kuwabwaga Chelsea watakaokuwa wageni wao katika mchuano ujao.

Kikubwa kinachomwaminisha Guardiola ni kwamba kufikia wakati kama huu msimu jana, Liverpool walikuwa wakijivunia pengo la pointi 10 zaidi kuliko wao kileleni mwa jedwali baada ya mechi 20 pekee za ufunguzi.

Ingawa hivyo, Man-City walisajili msururu wa matokeo bora yaliyowashuhudia wakipoteza alama tatu pekee katika jumla ya mechi 18 za mwisho wa muhula.

Kati ya mechi kubwa walizozitawala ni ile iliyowashuhudia wakizamisha chombo cha Liverpool uwanjani Etihad.

Wakicheza dhidi ya Liverpool wikendi iliyopita, Man-City walianza mechi kwa matao ya juu huku refa akiwanyima penalti ambayo kulingana na Guardiola walistahili kupewa baada ya Trent Alexander-Arnold kuunawa mpira sekunde chache kabla ya Fabinho kufungua ukurasa wa mabao wa Liverpool.

Kuhesabiwa kwa bao la Fabinho ni mojawapo ya matukio yaliyomkera pakubwa kocha Guardiola ambaye amewataka vinara wa EPL kuwachukulia hatua baadhi ya marefa ambao hutoa maamuzi mengi ya utata katika michuano muhimu.

Licha ya kupoteza mechi hiyo, Guardiola alikuwa mwingi wa sifa kwa vijana wake ambao kulingana naye, walijituma maradufu na kuonekana kuwazidi Liverpool maarifa katika takriban kila idara mwishoni mwa mechi.

“Haipingiki kuwa Liverpool ni miongoni mwa vikosi bora zaidi kwa sasa katika soka ya Uingereza na bara Ulaya. Ninawapongeza vijana kwa kujikakamua vilivyo ugenini. Si rahisi kwa kikosi chochote kuja uwanjani Anfield na kusakata soka safi kama walivyofanya vijana wetu,” akasema Guardiola.

Mabao mengine ya Liverpool ambao wameapa kunyanyua ufalme wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30, yalifumwa wavuni kupitia kwa Mohamed Salah na Sadio Mane kabla ya Man-City kufutiwa machozi na Bernardo Silva.

Rekodi ya Liverpool kwa sasa inarejesha kumbukumbu za 1993-94 ambapo Man-United walijivunia pengo la alama nane kileleni mwa jedwali la EPL baada ya mechi 12 pekee za ufunguzi wa msimu huo.

Licha ya masogora wake kuanza kupigiwa upatu wa kutawazwa mabingwa wa EPL muhula huu, Klopp amewataka vijana wake kuzimakinikia zaidi mechi zilizo mbele yao hasa ikizingatiwa ugumu wa ratiba itakayowakabili kati ya Novemba 23 na Januari 2. Kulingana na nahodha Jordan Henderson, matokeo ya Liverpool dhidi ya Man-City yanatosha kuwasadikisha mashabiki wao kuwa watawazwa mabingwa wa EPL msimu huu nchini ya kocha Klopp.

“Kikubwa zaidi kwa sasa ni kujitahidi kusajili matokeo bora katika kila mchuano. Sioni kitakachotuzuia kuweka hai matumaini ya mashabiki wetu iwapo tutajituma katika kila mechi jinsi tulivyofanya dhidi ya Man-City,” akasema Henderson katika kauli iliyotiliwa mkazo na Klopp.

Ushindi kwa Liverpool uliendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa mbele ya mashabiki wao wa nyumbani katika jumla ya michuano 49 iliyopita.

Katika matokeo ya mechi nyinginezo za EPL, Jumapili, Wolves waliwang’ata Aston Villa 2-1 nao Man-United wakawapepeta Brighton 3-1 uwanjani Old Trafford.

You can share this post!

TAHARIRI: Pia tuangalie faida za kongamano hili

Serikali yatangaza ufunguzi wa shule tano za Boni

adminleo