'Tangatanga' wadai Matiang'i alijua kitu kuhusu fujo za Kibra
CHARLES WASONGA
WABUNGE wa Jubilee wanaoegemea mrengo wa ‘Tangatanga’ sasa wamehusisha jina la Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i na Katibu katika wizara hiyo Karanja Kibicho na fujo zilizoshuhudiwa eneobunge la Kibra wiki jana.
Wakiongozwa na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa, wabunge hao wapatao 10 wamedai Jumanne kuwa siku moja kabla ya siku ya uchaguzi mdogo wa Kibra Mbw Matiang’i na Kibicho walikutana na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupanga njama kuhusu ghasia hizo.
“Tuna habari kwamba Odinga, Matiang’i na Kibicho walikutana katika hoteli moja mtaani Karen kupanga namna magenge ya wahalifu yangetumika kusababisha fujo katika uchaguzi huo. Kwa hivyo, magenge ya wahalifu waliowavamia wabunge Kibra yalikuwa na ulinzi kutoka kwa watu wanaohudumu katika ofisi ya Rais,” Bw Ichungwa amesema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.
Mbunge huyo alikuwa ameandama na wenzake Caleb Kositany (Soy), David Gikaria (Nakuru Mjini Mashariki), Ndindi Nyoro (Kiharu), Rigathi Gachagua (Karatina), Japhet Mutai (Bureti), Kagongo Bowen (Marakwet Mashariki), Jayne Kihara (Naivasha) miongoni mwa wengine.
Hata hivyo, wabunge hao hawajatoa ithibati yoyote kuthibitisha madai yao huku wakisema hawawezi kuandikisha taarifa kwa polisi kwa sababu “hatua hiyo haina maana yoyote.”
“Tunamtaka Waziri Matiang’i atoe taarifa kuhusu uhalifu uliotendeka katika eneobunge la Kibra. Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai pia anaeleza hatua ambazo amechukua dhidi ya vijana waliowashambuliwa mheshimwa Didmus Barasa na seneta wa zamani wa Kaunti ya Kakamega Dkt Boni Khalwale,” amesema Bw Kositany.
Amedai kuwa Bw Barasa ambaye ni Mbunge wa Kimilili amelazwa katika hospitali moja nchini Afrika Kusini baada ya kudungwa sindano ya sumu mnamo Alhamisi wiki jana ambayo ndiyo ilikuwa siku ya uchaguzi huo mdogo.