• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu wakosoa unyama wa polisi JKUAT

Viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu wakosoa unyama wa polisi JKUAT

Na LAWRENCE ONGARO

VIONGOZI wa wanafunzi wa vyuo vikuu wameitaka serikali kufanya hima kuwanasa maafisa wa polisi waliowajeruhi wanafunzi wa Chuo cha Kiufundi cha Jomo Kenyatta University of Agriculture and Technology (JKUAT), mnamo Jumatatu.

Na wakati huo huo Inspekta Mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai amekosa kuwataja maafisa wa polisi walionaswa kwenye kamera za siri za CCTV wakiwatandika wanafunzi kadha wa JKUAT, lakini badala yake akisema washukiwa hao wa kikosi cha polisi wataadhibiwa.

Wakiongozwa na kiongozi wa vyuo vya kiufundi nchini Bw Paul Karanja na Anne Mvuria, viongozi hao wameshutumu kitendo ambapo mwanafunzi mmoja wa JKUAT alichapwa na kujeruhiwa vibaya na polisi waliokuwa wakizima ghasia za wanafunzi.

“Polisi wamepewa jukumu la kuwalinda wananchi lakini ni aibu kuona ya kwamba wao ndio wanawakandamiza wananchi,” amesema Bw Karanja.

Amesema wanafunzi wa JKUAT kwa muda mrefu wamekuwa wakipitia masaibu mengi lakini hakuna hatua yoyote imechukuliwa na polisi.

“Mara nyingi wanafunzi hudungwa visu na wahuni wakati wanatoka shughuli zao na hata kuporwa fedha na vifaa vingine muhimu. Kwa hivyo, tunaitaka serikali ijitokeze wazi na kuona ya kwamba inalinda maisha ya kila mwananchi,” amefafanua kiongozi huyo wa wanafunzi.

Amesema Waziri wa Usalama na Mambo ya Ndani Dkt Fred matiang’i ameahidi ya kwamba hatua kali itachukuliwa dhidi ya afisa yeyote aliyehusika.

“Kwa hivyo tunataka hatua hiyo ichukuliwe mara moja bila kuchelewa. Iwapo hatua haitachukuliwa sisi kama viongozi wa wanafunzi tutafanya juhudi kuona ya kwamba wanafunzi wote kote nchini wanafanya maandamano ya pamoja ili serikali isikie matakwa yetu,” amesema kiongozi huyo.

Amesema pia wangetaka kupata nafasi ya kukutana na Rais Uhuru Kenyatta ili wamfahamishe masaibu yote wanayopitia kama wanafunzi wa vyuo vikuu.

“Tumekuwa tukipata matatizo mengi ambayo yamekosa kushughulikiwa na kwa hivyo tungetaka tupate nafasi ya kuwasilisha kwa Rais,” amesema kiongozi huyo wa wanafunzi.

Ilidaiwa mwanafunzi aliyejeruhiwa vibaya na polisi alipelekwa katika hospitali kuu ya Kenyatta ili kupata matibabu zaidi.

Wengine nao walipelekwa katika zahanati za karibu za eneo la Juja.

Naye kiongozi mwingine wa wanafunzi Bi Anne Mvuria amesema polisi wana jukumu la kulinda maisha ya kila mmoja bila kudhulumu na kukandamiza.

“Tunaitaka serikali ijitokeze wazi na kuona ya kwamba haki imetendeka kwa wanafunzi hao,” amesema Bi Mvuria.

Naye Mkurugenzi wa maswala ya ndani ya nchi Bw Chalton Murithi, amehakikishia waandishi wa habari kuwa tayari kuna uchunguzi unaoendelea na ifikapo Jumatano hatua itakuwa imechukuliwa mara moja.

“Tuko hapa kuona ya kwamba uchunguzi unafanywa kwa haki ili afisa yeyote aliyehusika na kitendo cha dhulma kwa mwanafunzi huyo achukuliwe hatua za kisheria,” amesema Bw Murithi.

Amesema tayari mkutano wa dharura ulikuwa ukiendelea kati ya chuo cha JKUAT na idara ya polisi ili kufanikisha uchunguzi huo mara moja.

Ametoa mwito kwa wananchi walio na habari yoyote inayoweza kusaidia polisi awasilishe mbele ili uchunguzi ufanywe.

You can share this post!

Rais wa zamani wa Amerika alazwa ili kufanyiwa uchunguzi wa...

Moto usiku wasababisha taharuki Mombasa Hospital

adminleo