• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Serikali kushtaki wazazi wa watoto katika ukahaba

Serikali kushtaki wazazi wa watoto katika ukahaba

Na MISHI GONGO

SERIKALI itawachukulia hatua wazazi wanaohimiza watoto wao kushiriki ngono na watalii kwa lengo la kujipatia pesa.

Mratibu wa Ukanda wa Pwani, Bw John Elungata, alisema hatua hii ni kuzuia visa vya wazazi kuwatumia watoto wadogo katika ukahaba ili kujipatia pesa kutoka kwa watalii wanaozuru Pwani.

Alisema baadhi ya wasichana hutoka kaunti zingine na kusafiri maeneo ya Pwani kwa lengo la kushiriki mapenzi na watalii.

“Tumekuwa tukishuhudia visa vya watalii kutumia watoto wadogo kimapenzi na tabia hii hatutaikubali.Tunataka wazazi wazingatie majukumu yao kikamilifu,”alisema.

Aliwaomba wazazi kutumia muda huu kuwaelekeza watoto wao kuhusu masuala ya kidini miongoni mwa mengine yanayofaa.

Bw Elungata alisema kuna baadhi ya watoto wa kike ambao hushawishiwa na wenzao kushiriki biashara hiyo ili kujipatia pesa za haraka.

Pia alisema kuna baadhi ya wazazi ambao hutumia watoto wao kama vitega uchumi.

Afisa mkuu katika idara ya watoto kaunti ya Mombasa, Bw Philip Nzenge, alisema idara yake itashirikiana na maafisa wa polisi kuhakikisha wanachukua hatua dhidi ya watu wanaohusisha watoto kwa mambo yasiyofaa.

Alieleza kuwa wazazi watakaotembelea vilabu vya pombe wakiwa na watoto watachukuliwa hatua pamoja na wamiliki wa vilabu hivyo.

“Mzazi unafaa kumlinda mwanao wakati wote.Si vyemai kuona mtoto katika kilabu cha pombe usiku wa manane. Utovu wa nidhamu hutokea sehemu hizi na watoto huiga ndiposa kumekuwa na ongezeko la mimba za mapema,dhuluma za kimapenzi na watoto kutumia vileo katika kaunti hii,” alisema Bw Nzenge.

Aliongeza kuwa hoteli nyingi mjini Mombasa hazijaweka mikakati ya kulinda haki za watoto.

You can share this post!

Watahiniwa 34 waandamwa na vituko KCSE ikiendelea

Upinzani mkali katika kongamano la uzazi

adminleo