• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
UNFPA yataka dhuluma dhidi ya wanawake katika jamii zikome

UNFPA yataka dhuluma dhidi ya wanawake katika jamii zikome

Na Pauline Ongaji

MMOJA kati ya wanawake watatu duniani hushuhudia dhuluma za kijinsia kutoka kwa wapenzi au waume zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu (UNFPA), Dkt Natalia Kanem, aliambia kongamano la Kimataifa kuhusu Idadi ya watu na Maendeleo (ICPD), alisema unyama huo unachukuliwa kuwa jambo la kawaida.

Kwenye kongamno hilo linalotarajiwa kumalizika leo katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa KICC, wajumbe walichukua muda kuwakumbuka wahanga wa dhuluma za kijinsia. Ilifichuliwa zaidi kwamba kila siku, wanawake na wasichana 137 huuawa na jamaa zao.

Kuhusiana na takwimu hizo, Dkt Kanem alisema kwamba haitakuwa haki ikiwa jamii ya kimataifa itaendelea kukaa kimya huku wanawake wakiendelea kudhulumiwa.

“Ndiposa tunashirikiana na mradi wa Spotlight Initiative ili kukabiliana na aina zote za dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana,” aliongeza.

Pia akizungumza kwenye kikao hicho, Bi Gita Sen, profesa wa hazina ya afya ya umma nchini India, alisema kwamba 58% ya dhuluma dhidi ya wanawake hutekelezwa na wapenzi, waume, au jamaa zao.

“Hii ni kumaanisha kwamba nyumbani ndio sehemu hatari zaidi kwa mwanamke.”

Bi Phumzile Mlambo- Ngucka, Mkuregenzi Mtendaji wa UN Women alisema kwamba kunyimwa uwezo wa kiuchumi kumewafanya wanawake kuwategemea sana wanaume, suala linalowaweka katika hatari zaidi ya kukumbana na dhuluma.

Kuligana na Bi Mlambo, serikali zinapaswa kuhakikisha kuwepo kwa taasisi za kuwapigania na kuwalinda wanawake dhidi ya dhuluma za kijinsia.

“Kuna haja ya kuwepo kwa mifumo thabiti ya kufanya hiyo katika mataifa yote. Mifumo hii inahusisha ushirikiano wa polisi, idara ya mahakama na jamii kwa ujumla,” alisema.

Ni hoja iliyoungwa mkono na Bw Rasmus Prehn,Waziri wa ushirika wa ustawi wa Denmark, aliyesema kwamba kunapaswa kuwa na sera za kukabiliana na dhuluma za kijinsia.

“Ikiwa mataifa yatafanya bidii kupunguza viwango vya umaskini na kuimarisha ufikiaji wa elimu, huenda hii ikapunguza kabisa visa vya dhuluma za kijinsia,” alisema Kwa upande mwingine, Waziri Prehn alisisitiza kwamba kuna haja ya wanaume pia kuhusishwa katika vita dhidi ya dhuluma za kijinsia.

“Hii ni muhimu hasa katika mazingira kama nchini mwangu ambapo licha ya kwamba viwango vya umaskini viko chini, bado visa vya dhuluma za kijinsia vinaendelea kuripotiwa,” aliongeza.

You can share this post!

Utata kuhusu mwanamume aliyedandia ndege maiti yake...

Jinsia: Kenya yaorodheshwa moja ya nchi 50 bora duniani

adminleo