TAHARIRI: Sonko aondoe mzaha katika usimamizi wa kaunti
NA MHARIRI
KAUNTI ya Nairobi ina fahari na jivunio kubwa la kuwa mji mkuu wa nchi wenye serikali kuu inayoendesha shughuli anuwai za nchi.
Ni jiji kuu lenye mvuto na sifa tele kutoka kwa jamii ya kimataifa kutokana na vivutio mbalimbali vya kitalii.
Hivyo basi, pana haja ya kaunti hii kuwa kielelezo bora kwa kaunti nyinginezo kuhusu usimamizi na uendeshaji wa shughuli zake kwa ujenzi wa taifa.
Haihalisi kabisa kuona mitafaruku, mizozo na migogoro mingi inayoonyeshwa kupitia kwa madiwani na viongozi wengine wa kaunti. Kadhia hii inashusha kwa asilimia kubwa staha na hadhi ya jiji la Nairobi.
Yakini, kaunti ya Nairobi inaelekea kutwaa nafasi ya kwanza kwa uongozi uliofeli.
Kwanza, ni nadra sana kumpata Gavana Sonko katika ofisi yake ya City Hall, na hata ingawa anadai kufanya hivyo ili kulinda usalama wake, hiyo si sababu tosha ya kukosekana kwake ofisini hali ikiendelea kuvurugika.
Kukosekana kwake huko kunashadidiwa na ukweli kwamba Kaunti ya Nairobi haina naibu gavana kwa zaidi ya miaka miwili sasa, na inavyodalilisha, Sonko hana nia ya kuteua mtu kuwa naibu wake.
Mwezi Septemba mwaka jana, baadhi ya madiwani waliungana kwa juhudi za kumng’oa mamlakani kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Spika Beatrice Elachi ambaye alirejeshwa na mahakama.
Si hayo tu, madiwani hao walihiari kutozingatia maagizo ya mahakama walipojaribu kumtimua ofisini kwa mara ya pili mwezi jana.
Hata hivyo, linalojitokeza kwa sasa ni kwamba MCAs hao sasa wamejigeukia na kugongana wao kwa wao. Mnamo Jumatatu wiki hii, walitumia poda ya pilipili na vitoa machozi kuonyeshana ubabe wa kisiasa.