Hatumjui, KAA yakana habari za Mkenya aliyedondoka London
Na BENSON MATHEKA
MAMLAKA ya kusimamia viwanja vya ndege nchini (KAA), imekanusha habari za shirika la habari la Sky News la Uingereza kwamba mwili wa mwanamume ulioanguka kutoka kwa ndege mjini London ulikuwa wa mfanyakazi wa kampuni inayohudumu katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Kampuni ya Colnet ambayo shirika hilo lilisema mwanamume huyo alikuwa akifanyia kazi, pia lilikanusha habari kwamba alikuwa mfanyakazi wake.
Kauli ya KAA na Colnet inatofautiana na Mamlaka ya Safari za Ndege nchini ambayo awali ilisema huenda mwanamume huyo alikuwa mfanyakazi kampuni moja ya kudumisha usafi katika uwanja huo.
Hata hivyo, usalama katika uwanja huo unatiliwa shaka kufuatia kisa hicho maswali yakiibuka jinsi mwanamume huyo aliweza kuingia uwanjani na kufikia ndege.
Sky News ilimtambua mwanamume huyo kama Paul Manyasi, aliyekuwa akifanya kazi katika kampuni ya Colnet, lakini kulingana na KAA na kampuni hiyo, jina hilo haliko katika sajili ya kidijitali ya watu wanaohudumu katika uwanja huo.
“Maafisa wa usalama kutoka vitengo tofauti walianza uchunguzi kuhusiana na madai katika makala ya Sky News kwamba mwanamume ambaye mwili wake ulianguka kutoka kwa ndege alikuwa akifanya kazi katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta na inataka kusema uchunguzi huo unaendelea kwa kuzingatia habari zote zitakazopokelewa,” KAA ilisema kwenye taarifa.
Mkurugenzi wa Colnet, Bw Chege Kariuki, alisema kampuni ilishangazwa na ripoti ya Sky News. “Tunashangazwa na habari zilizopeperushwa na Sky News Network zinazohusisha Colnet limited na mwanamume huyo,” Bw Kariuki alisema kwenye taarifa.
Alisema kampuni iliwasilisha rekodi na habari za wafanyakazi wake wote kwa wachunguzi ambao wanaweza kuthibitisha haina mfanyakazi kwa jina Paul Manyasi.
Kampuni hiyo iliwataka watu wanaodai kuwa na habari kuhusu mtu huyo kurekodi taarifa kwa polisi.
Mnamo Jumanne, runinga ya Sky TV ilipeperusha ripoti zilizodai kuwa mwanamume huyo alifahamika kama Paul Manyasi na kwamba alikuwa akifanya kazi katika kampuni ya Colnet inayotoa huduma za usafi katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta.Iliwahoji watu kadhaa akiwemo baba yake Isaac Manyasi, aliyesema kwamba hakuwa amepokea habari zozote kumhusu mwanawe.
Baadhi ya watu waliohojiwa wakiwemo wafanyakazi wa kampuni hiyo walisema walifahamishwa kwamba mmoja wao alitoweka mwishoni mwa Juni mwaka huu na wakaagizwa kutofichua habari hizo.
Mwanamke aliyedai kuwa mpenzi wa mwanamume huyo alieleza ripota wa Sky News kwamba alienda kazini siku hiyo na hakurudi.
Mwezi jana, polisi wa Uingereza walitoa picha wakitarajia kuwa ingesaidia kutambua mwanamume huyo na familia yake kufahamishwa.
Aidha, walichapisha picha za bidhaa ambazo mwanamume huyo alikuwa nazo.Mwili wa mwanamume huyo unahifadhiwa katika mochari moja Uingereza hadi uchunguzi utakapokamilika.