Makala

KILIMO NA BIASHARA MASHINANI: Kilimo cha mboga za aina tofauti kimesaidia aweze kulipia wanawe karo

November 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES ONGADI

WAKULIMA wengi Kaunti ya Kisumu walikuwa na dhana kwamba kilimo cha mboga hakiwezi kushamiri kama ilivyo kwa kilimo cha miwa, pamba na mpunga.

Japo baadhi walilima mboga na matunda eneo hili lakini shingo upande, hawakuamini kwamba kiliweza kuwa kitega uchumi kwao.

Hata hivyo, Bi Mary Odenya kutoka kijiji cha Kamagaga, lokesheni ya Ombeyi kaunti ndogo ya Muhoroni, aliamua kuvalia njuga kilimo cha mboga aina mbali mbali .

“Wengi hapa waliamini kuwa kilimo cha mpunga na miwa pekee ndicho kinaweza kuwakwamua kiuchumi,” anasema Mary ambaye ni mjane.

Kulingana naye, maisha yalibadilika mumewe alipofariki 1991.

Aliwaza na kuwazua jinsi ambavyo angewalea wanawe ambao ndio walikuwa wako shule za chekechea na msingi.

“Nilianza maisha magumu kwa kuajiriwa kama mpishi katika mojawapo ya shule ya upili eneo hili kwa mshahara wa ksh 4,500 kwa mwezi,” anasema.

Hata hivyo, kadri miezi na miaka ilivyoyoyoma ndivyo maisha yalivyozidi kuwa magumu huku akikosa fedha za kuwalipia karo wanawe ambao walikuwa katika shule za upili.

Mnamo 2001, aliamua kujitosa kikamilifu katika kilimo cha mboga akianza na sukumawiki, lengo likiwa kujiinua kiuchumi.

Lakini mambo hayakumwendea vyema katika miaka ya mwanzo hadi pale alipoamua kusaka ushauri kutoka kwa wataalam wa kilimo eneo la Kisumu.

Anasema, mambo yalianza kumnyookea punde alipoanza kufuata kanuni za kilimo cha mboga hasa sukumawiki.

Kabla ya kupanda sukumawiki shambani, Mary huhakikisha ametengeza miche kwa kipindi cha siku 21.

Ni baada ya kumalizika kwa kipindi hicho ndipo anaipanda shambani huku akiwacha nafasi ya futi moja kutoka shimo moja hadi lingine na upana wa futi moja unusu. Kupata mboga za kuvutia na zinazonawiri, anatumia mbolea aina ya Sulphate na Urea.

Changamoto inayomkabili ni aina ya wadudu wanaotoboa matawi ya mboga hasa kipindi inapokaribia kukomaa.Anatumia dawa aina ya Halothin kuwakabili wadudu hao.

Shamba la sukumawiki la Bi Mary Odenya lililoko kijiji cha Ombeyi, Kaunti ya Kisumu. Picha/ Charles Ongadi

Ukosefu wa maji wakati wa kiangazi pia hutatiza kilimo chake na wakati mwingine hulazimika kukodisha mashine ya kuvuta maji kutoka mto ulio karibu na kunyunyizia shambani mwake.

Kulingana na Mary, mboga za sukumawiki huchukua siku 21 pekee kuanza kuvunwa na kipindi cha kati ya mwaka hadi miaka miwili ikiendelea kuvunwa.

Mara baada ya kuanza kupata faida katika kilimo cha sukumawiki, alijitosa katika kilimo cha mboga za kienyeji kama sagaa, mchicha na mnavu.

“Wengi wamebadilisha mtindo wao wa kula wakizingatia sana mboga za kienyeji jambo ambalo limenipatia faida na kuweza kubadilisha maisha yangu na familia yangu,” anaeleza.

Anavuna mara mbili kwa wiki ambapo anatia kibindoni kiasi cha Sh3,800 kwa sukumawiki, Sh2,500 kwa sagaa, Sh2,400 za mchicha na Sh 1600 kwa mboga za mnavu.

Wateja wake hufika asubuhi na mapema kila siku ya mavuno na kumrahishia mwendo wa kufika sokoni ama kuchuuza kwa wateja wake.

Kati ya mafanikio aliyoyapata hadi kufikia sasa katika kilimo cha mboga ni kwamba anawalipia karo wanawe wawili ambao ni watahiniwa wa Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu na mmoja aliye katika chuo kikuu.

“Nawahimiza akina mama wenzangu hasa wajane eneo hili wasiketi wakisubiri kusubiri kuletewa kila kitu na warithi bali kujizatiti kwa kilimo ambacho ni uti wa mgongo maishani,” anasema.

Kwa sasa mama huyu ana mipango ya kukodisha shamba ekari moja zaidi ili kupanua kilimo chake.