Isuzu yamtuza Eliud Kipchoge gari jipya lenye thamani ya Sh4.1 milioni
Na AYUMBA AYODI
ISUZU East Africa hatimaye imemtuza bingwa wa marathon mbio za Olympic Eliud Kipchoge, gari jipya aina ya Isuzu Single Cabin lenye thamani ya kiasi cha Sh4.1 milioni Jumamosi baada ya ufanisi mkubwa wa kuwa binadamu wa kwanza kukimbia mbio za marathon kwa muda chini ya saa mbili za ‘Ineos 159 Challenge’ Oktoba 2019.
Mwenyekiti wa kampuni ya Isuzu World ambayo ni maarufu kwa uundaji, utengenezaji na ukarabaiti wa magari Eisaku Akazawa amekuwa nchini akitokea Japan ili kumtuza Kipchoge katika hafla iliyoandaliwa katika Msitu wa Karura.
Hii ilikuwa ni baada ya mwanariadha huyo aliyekuwa na mkewe Grace pamoja na watoto wao watatu, kuongoza washiriki wapatao 200 wakiwemo wanafunzi, kukimbia umbali wa kilomita nne hapo Karura.
Amekuwepo kocha wake Patrick Sang, mwenzake katika mazoezi Geoffrey Kamworor ambaye majuzi alishinda mbio za New York City Marathon, Sally Chepyego aliyemaliza wa tatu katika mbio za Berlin Marathon na bingwa wa mwaka 2015 wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji Hyvin Kiyeng.
Mnamo Oktoba 12, 2019, Kipchoge alitumia muda wa 1:59:41 kukamilisha mbio za “Ineos 1:59 Challenge” jijini Vienna, Austria.
Gari alilotuzwa lina nambari za usajili KCW 159V, ambapo “159V” inaendana na muda wa saa 1:59 na V kuwakilisha jiji la Vienna.
Akazawa, alikuwa na meneja mkurugenzi wa Isuzu East Africa, Rita Kavashe.
“Ninamualika Kipchoge katika kiwanda chetu Japan kuwapa motisha wafanyakazi wetu,” amesema Akazawa akisifu bidii, nidhamu na moyo wa kujituma alioonyesha Kipchoge.
Kipchoge, licha ya kushinda taji la dunia la mbio za mita 5000 mwaka 2003 akiwa na umri wa miaka 19, aling’ang’ana sana kabla ya kushinda dhahabu katika mbio za Marathon za mashindano ya Olympic jijini Rio de Janeiro mwaka 2016.
“Inabidi kujituma kwani hakuna binadamu ambaye amewekewe ukomo wa aina fulani – No Human is Limited – na kwamba kwa vijana ni muhimu pia kuzingatia elimu,” amesema Kipchoge.
Naye Kavashe ametaja sababu ya kualika wanafunzi wakiwemo wa Shule ya Sekondari ya Muhuri Muchiri na Embakasi Girls kuwa ni kuwapa motisha.
“Tumetaka wajionee wenyewe kuwa mtu akijiamini maishani kuufikia ufanisi linakuwa ni jambo rahisi,” amesema Kavashe.