• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:07 PM
Wakulima wavuruga kikao cha jopokazi la kahawa

Wakulima wavuruga kikao cha jopokazi la kahawa

Na GEORGE MUNENE na DAVID MUCHUI

MKUTANO uliokuwa umeitishwa na Jopokazi Malum Kuhusu Kahawa ulitibuka mnamo Ijumaa, baada ya wakulima katika Kaunti ya Kirinyaga kuuvuruga.

Mkutano huo ulikuwa umepangiwa kufanyika katika Kanisa la Kianglikana (ACK) Kutus kujadili masuala yanayoikumba sekta ya kahawa, lakini wakulima hao wakasema kuwa hawana imani na jopo hilo.

Kizaazaa kilianza pale wakulima walianza kuingia katika ukumbi wa kanisa hilo, huku wanachama wa jopo wakijitayarisha kuuanza rasmi.

Wakulima waliwakejeli maafisa hao na kuwaambia kuondoka mara moja la sivyo wawakabili.

Kwa kuhofia usalama wao, maafisa hao waliondoka haraka na kwenda mahali kusikojulikana.

Baada yao kuondoka, wakulima hao kutoka vyama mbalimbali vya ushirika katika eneo hilo walianza kusherehekea.

Walililaumu jopo hilo kwa kukosa kujumuisha maoni yao kwenye ripoti yake.

“Wakati maafisa hao walizuru eneo hili mwaka uliopita na kuwaambia yale tungetaka yatekelezwe ili kuleta katika mageuzi sekta hii, hawakuyajumuisha maoni yetu hata kidogo. Hatutaki kusikia lolote kuihusu,” akasema Bw Francis Kiura, ambaye ni mmoja wa wakulima hao.

Zaidi ya hayo, walilalama kuwa eneo hilo halijajumuishwa kwenye jopokazi hilo.

“Hatuna mkulima hata mmoja kutoka eneo hili katika jopokazi hilo. Tumebaguliwa, hivyo hatutaikubali ripoti yake,” akaongeza Bw Kiura.

Awali, maafisa waliwalaumu wakulima kwa kutofahamu ukweli.

“Wakulima wangengoja kutusikiliza kabla ya kuzua vurugu. Wanapinga mambo wasiyoyafahamu,” akasema mmoja wa wanajopo hao.

Kwingineko, Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri ameteua watu 13 kuhudumu katika Jopokazi la Utekelezaji wa Ripoti Kuhusu zao la Miraa.

Jopokazi hilo litahudumu kwa mwaka mmoja.

Tangazo rasmi

Kwenye tangazo lililowekwa katika gazeti rasmi la serikali Ijumaa, Bw Kiunjuri alisema kuwa jopokazi hilo litaongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo Dkt Andrew Tuimur.

Wanachama wa jopo hilo wanajumuisha Mabwana Kobia Michubu, Joseph Mutharimi, Morgan Kiogora, Dave Ntawa, Kimathi Munjuri, Jervasius Nyombyekothe, Rufus Miriti, John Mukiira, Danson Mwangangi, Clement Muyesu, Stephen Kubai, Dkt Elijah Kathurima na Bi Anne Nyaga.

Uteuzi huo unajiri huku kukiwa na hofu kwamba bajeti ya zao hilo mwaka huu imepunguzwa hadi Sh400 milioni.

Vilevile, kumekuwa na malalamishi kutokana na ucheleweshaji katika utekelezaji wa miradi ya maji na soko ambayo ilitengewa fedha mwaka uliopita katika kaunti za Meru, Embu na Tharaka Nithi.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakuzaji Miraa cha Nyambene Bw Kimathi Munjuri alilalamikia ucheleweshaji katika kumaliza visima vilivyoanzishwa mwaka 2018.

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Polisi wa kwanza wa kike nchini...

Miili inayoaminika ni ya mwanamke na wanawe wawili...

adminleo