HabariSiasa

Boma la Rais lapasuka zaidi

November 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NDUNG’U GACHANE Na BENSON MATHEKA

MKUTANO wa wiki iliyopita kati ya Rais Uhuru Kenyatta na viongozi wa Mlima Kenya katika ikulu ndogo ya Sagana ulionuiwa kuzima tofauti katika chama cha Jubilee, umeacha jamii ya Gema ikiwa imegawanyika hata zaidi.

Baadhi ya wanasiasa wanasema mkutano huo haukufanikisha ajenda ya kuwaleta pamoja viongozi wa eneo hilo.

Baadhi ya maseneta, wabunge na magavana wanasema viongozi waliochaguliwa hawakutambuliwa katika mkutano huo huku walioshindwa kwenye uchaguzi wakipatiwa nafasi kuhutubu.

Walisema mkutano huo ulipangwa na maafisa wa ikulu ambao wamekuwa wakimpa Rais mwongozo usiofaa wa kuwaamrisha viongozi wanaoegemea mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto kuunga mkono ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Wabunge wanaomuunga Dkt Ruto, maarufu kama Tanga Tanga hawakupatiwa nafasi ya kuhutubu wakiwemo wanaotoka Kaunti ya Nyeri ambako mkutano ulifanyika.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria alisema mkutano huo haukuafikia lolote, akisisitiza lengo kuu lilikuwa ni kuwaaibisha viongozi waliochaguliwa na kudhihirisha kwamba serikali ina viongozi teule ambao wanatarajiwa kutekeleza ajenda zake ikiwa ni pamoja na kuvumisha BBI.

Mbunge huyo alisema viongozi waliochaguliwa hawakuheshimwa ikizingatiwa waliohutubu walitoa kauli zao kimakusudi kuashiria kwamba wanaunga mkono BBI.

“Kuna baadhi ya watu ambao wanatia doa uongozi wa Rais kwa kumshauri visivyo kuhusu masuala yenye umuhimu kwa taifa hili. Viongozi waliochaguliwa walidharauliwa na hata hakukuwa na mfumo ulioeleweka wa viongozi kuketi,” akasema Bw Kuria kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Kulingana naye, mkutano huo ulipangwa na wandani wa Rais ambao wamekerwa na wimbi la mabadiliko linaloendelea kushuhudiwa eneo la Kati, akisema hali kama hiyo pia ilitokea wakati marais wa awali walipokaribia kuondoka mamlakani wandani wao walipojaribu kuwalazimisha raia kukumbatia mkondo wao wa kisiasa.

“Hawa wanaomwelekeza Rais vibaya wanafaa kufahamu kwamba wakati wa mabadiliko umefika. Enzi za utawala wa Jomo Kenyatta walijaribu kubadilisha katiba ili kuzuia mambo ambayo kimaumbile yangetokea tu. Kwa sasa tunaathirika na matukio sawa ambayo pia yalishuhudiwa katika utawala wa Mzee Kibaki ukitamatika,” aliongeza Bw Kuria.

Pia alimshutumu Rais Kenyatta kwa kujitetea kwamba hakuchaguliwa pekee yake kuwahudumia wakazi wa eneo hilo.

“Nimesikia kuhusu yale mnasema kuhusu kahawa, chai, pareto na mengine mengi. Ninatambua kwamba watu hawakunichagua pekee yangu na siwezi kusuluhisha shida zote pekee yangu. Lazima tufanye kazi pamoja,” akasema Rais Kenyatta kwenye mkutano huo.

Bw Kuria alimtaka Rais kueleza taifa namna anavyotumia bajeti ya Sh3 trilioni kabla ya kuwaandama wabunge ambao huwa na bajeti ya Sh100 milioni pekee.

“Mimi huwa nina Sh100 milioni kwenye Hazina ya Kitaifa ya Fedha za Maeneobunge (CDF) huku Rais akiwa na Sh3 trilioni. Tunafaa kumuuliza ametumia pesa hizo vipi?’’ akasema.

Mbunge wa Bahati, Kimani Ngunjiri naye alimshutumu Rais kwa kufanya kazi na viongozi walioshindwa kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

“Bado sielewi kwa nini Rais anafanya kazi na viongozi ambao hawakuchaguliwa. Mutahi Kagwe hakuchaguliwa ilhali alitekeleza wajibu muhimu kwenye mkutano. Bi Sabina Chege ni Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Murang’a na ndiye alifanywa mwenyeji badala ya mbunge wa eneo hilo Rigathi Gachagua,” akasema Bw Ngunjiri,

“Kwangu mkutano huo uliwagawanya viongozi zaidi kwa sababu Rais hakutelekeza ahadi yake ya kufanya kazi na viongozi waliochaguliwa. Hata katiba inatambua tu viongozi waliochaguliwa kuwa wenye usemi kwa niaba ya wananchi,” akaeleza.

Baadhi ya maseneta na magavana walidai kwamba mkutano huo sasa umefungua ukurasa wa mapambano kati ya viongozi wakongwe na wale chipukizi.