Habari MsetoSiasa

Ruto amtafute Mzee Moi amsamehe – Atwoli

November 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA TITUS OMINDE

KATIBU Mkuu wa Muungano wa wafanyikazi nchini (COTU), Bw Francis Atwoli amemtaka Naibu Rais William Ruto kumtafuta kwa hali na mali rais mstaafu Daniel Moi ili amfanyie matambiko apate baraka za kumwezesha kuwa rais.

Akihutubu katika ngome ya Dkt Ruto katika kituo cha biashara cha Ilula, Kaunti Uasin Gishu, Bw Atwoli alisema uhusiano tata kati ya Naibu Rais na familia ya Moi ni sawa na laana ambayo itamzuia Bw Ruto kunawiri kisiasa.

Bw Atwoli alidai kuwa iwapo Dkt Ruto hatanyenyekea na kumtafuta Mzee Moi kumfanyia matambiko na kuomba amsamehe, kamwe hatapata nafasi ya kuongoza nchi hii.

“Mimi kama mzee ninataka kumwambia Dkt Ruto kwamba iwapo angependa kupata baraka lazima anyenyekee na kumtafuta Mzee Moi hata kama ni usiku ili amuombe msamaha akiwa angali hai,” akasema Bw Atwoli

Kwa kejeli, Bw Atwoli alisema Dkt Ruto ni kijana mzuri lakini kiburi na kuwakosea wazee heshima ndicho kizingiti kikubwa ambacho anapaswa kujiepusa nacho.

Kwa mara nyingine Bw Atwoli alisifu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) na kusema kuwa Wakenya wataiunga mkono, hata ingawa haijatolewa

“BBI tayari imepita na wale ambao wanaipinga wajue mapema hiyo ni lazima itapita,” akasema Bw Atwoli

Msimamo wa Bw Atwoli uliungwa mkono na mbunge wa Cherangany, Joshua Kutuny ambaye alirai jamii ya Wakalenjin kuunga mkono BBI badala ya kuingiza siasa za kijamii.

“Wakati umefika kwa watu wetu kutumia busara na kuunga mkono BBI kama njia moja ya kuonyesha ukomavu wa demokrasia katika jamii bila kutegemea mtu mmoja kutuamulia,” akasema Bw Kutuny.