• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KCPE: Wanafunzi kufahamu shule watakazojiunga nazo Desemba 2

KCPE: Wanafunzi kufahamu shule watakazojiunga nazo Desemba 2

NA CECIL ODONGO

WANAFUNZI 1,083,456 waliofanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE), ambao matokeo yake yalitolewa Jumatatu, watafahamu shule za upili ambazo watajiunga nazo kufikia Desemba 2.

“Tutatumia mtindo ambao ulitumika mwaka jana ili kuhakikisha kila moja anajiunga na shule kulingana na alama alizopata,” akasema Waziri wa Elimu, Prof George Magoha.

Alisema serikali ikishirikiana na wafadhili imetenga Sh8 bilioni za kuimarisha miundomsingi na kujenga madarasa mapya katika shule za upili ili kutosheleza idadi kubwa ya wanafunzi.

Uteuzi wa wanafunzi wa kujiunga na shule za upili miaka ya nyuma umekuwa ukizua malalamiko kutoka kwa wamiliki wa shule za kibinafsi wakidai kwamba wanafunzi wa shule za umma hupendelewa.

Wanafunzi 9,770 ambao walipata alama 400 na zaidi wana nafasi nzuri ya kujaza nafasi katika shule za kitaifa katika maeneo mbalimbali nchini.

Prof Magoha pia alisisitiza kwamba wizara imeamua kuteua shule za upili kwa wanafunzi wa mwaka huu mapema ili kuwapa wazaz muda wa kujitayarisha.

Kuhusu Mtaala mpya wa CBC, Prof Magoha alitangaza kwamba serikali imewekeza Sh14 bilioni ambazo zitatumika kununua na kuchapisha vitabu kwa ajili ya wanafunzi watakaojiunga na gredi ya nne.

“Kufikia Disemba 17, vitabu vyote vinavyohitajika kwa wanafunzi wanaojiunga na gredi 4 vitakuwa vimesambazwa katika shule zote nchini. Mtaala huo mpya unaendelea kupata ufanisi na mnamo Januari 6 wanafunzi watajiunga na gredi 4,” akaongeza Prof Magoha.

Alisisitiza kwamba wizara yake imehakikisha kwamba kila mwanafunzi kutoka shule ya msingi na upili anapata vitabu vya kutosha badala ya kitabu kimoja kutumika na wanafunzi wengi.

Vilevile alitangaza kwamba wanafunzi 9,000 watapata ufadhili wa masomo na watakaolengwa zaidi ni watoto kutoka mitaa ya mabanda katika miji mikuu.

You can share this post!

Shangwe kijijini mwanafunzi kuongoza #KCPE2019 kwa alama 440

KCPE: Matokeo ya wanafunzi walemavu yaimarika

adminleo