Macharia aamriwa kufika mbele ya maseneta

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wamemtaka Waziri wa Uchukuzi James Macharia kufika mbele yao ndani ya wiki mbili kujibu maswali kuhusu kusambaratishwa kwa uchukuzi wa barabarani kufuatia amri iliyotolewa na wizara yake kwamba bidhaa kutoka Mombasa hadi maeneo ya bara zisafirishwe kwa garimoshi kupitia reli ya kisasa, SGR.

Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Uchukuzi, Kimani Wamatangi alitoa uamuzi huo baada ya Bw Macharia kufeli kuhudhuria mkutano baina ya wanachama wa kamati hiyo na wasafirishaji bidhaa.

Pia alisema kuwa Wizara ya Uchukuzi ndiyo italipia gharama ya usafiri ya wachukuzi hao wa mizigo katika siku mbili ambazo walisafiri kutoka Mombasa hadi Nairobi kukutana na maseneta pamoja na Waziri Macharia kuhusu amri hiyo ya serikali.

Miezi miwili iliyopita Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) na ile ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) zilitoa amri kwamba mizigo yote iliyoagizwa kutoka nje na inayonuiwa kupelekwa bara itasafirishwa kwa SGR hadi Nairobi kuanzia Agosti 7.

Ajira zapotea

Hatua hiyo iliathiri biashara za kampuni za kusafirisha mizigo kutoka Mombasa hadi maeneo ya bara na ni hali iliyowaacha wafanyakazi wengi bila ajira.

“Tumeamua kwamba Waziri pamoja na wakurugenzi wake wa Mamlaka ya Kusimamia Barabara Kuu (KeNHA), ile ya kusimamia barabara za vijijini (KeRA) na Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) watahitajika kufika mbele ya kamati hii ndani ya muda wa siku 14,” akasema Bw Wamatangi.

Bw Macharia amekuwa akikwepa kufika mbele ya kamati hiyo huku akisalia kimya kuhusu masaibu ya wachukuzi wa mizigo ambao wamekosa ajira baada ya kutolewa kwa amri hiyo miezi mitatu iliyopita.

Treni ya mizigo ya Madaraka Express inayotumia SGR imekuwa ikijizatiti kuvutia wasafirishaji mizigo tangu kuzinduliwa kwa huduma hiyo mapema mwaka 2018 lakini haijafaulu.

Hii ji kutokana na kile wadau wanasema ni ada za juu zinazotozwa na treni hiyo kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Mombasa na eneo la kuhifadhi makasha eneo la Embakasi, Nairobi.

Wanachama wa muungano wa kimataifa wa wasafirishaji bidhaa, tawi la Kenya wamekuwa wakiandaa maandamano Mombasa kila wiki kuishinikiza serikali kufutilia mbali amri hiyo.

Habari zinazohusiana na hii