StandChart yaagizwa itoe ushahidi katika wizi wa Sh827m
Na RICHARD MUNGUTI
BENKI ya Standard Chartered (SCB) ilipewa wiki mbili na mahakama ya kuamua kesi za ufisadi kuwasilisha stakabadhi za kifedha za kampuni ya Pipeline Company (KPC) ambayo mkurugenzi mkuu (MD) wake wa zamani Dkt Shem Ochuodho ameshtakiwa na wengine wawili kwa ulaghai wa Sh827 milioni.
Hakimu mkuu Douglas Ogoti alitoa agizo hilo baada ya kuelezwa na wakili wa SCB Dkt Davison Mwaisaka hati za benki huharibiwa baada ya miaka saba.
“Ulifika kortini kueleza ziliko stetimendi za benki za kampuni ya KPC wakati Dkt Ochuodho alipokuwa MD,” Bw Ogoti alimweleza Dkt Mwaisaka.
Dkt Ochuodho ameshtakiwa pamoja na Terry Winjenje na kampuni yaTriple A Capital iliyodai ilikuwa inaisaidia KPC kupata mikopo ya kujistawisha kutoka mataifa ya ng’ambo.
Dkt Mwaisaka aliambia mahakama kuwa SCB huharibu hati zake zote kuhusu uwekaji na utoaji wa pesa baada ya miaka saba.
“Je, hampigi picha hati zote na kuziweka,” akamwuliza Bw Ogoti.
Akijibu Dkt Mwaisaka alisema kuwa baada ya miaka saba hati zote huharibiwa hata zile zimewekwa katika mitandao ya PDF.
Afisa huyo aliomba muda wa wiki mbili benki ikazitafute hati hizo na “ikiwa ziliharibiwa basi atawasilisha cheti cha kuonyesha ziliharibiwa,”
Bw Ogoti aliamuru kesi hiyo itajwe Desemba 9, 2019 Dkt Mwaisaka aeleze mahakama ikiwa ushahidi unaotakiwa kama umepatikana.
Hakimu alisema iwapo nakala asili hazipo basi itabidi nakala za fotokopi zitumike.