• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 8:55 AM
SHAIRI: Athari za vileo na mihadarati

SHAIRI: Athari za vileo na mihadarati

Na KULEI SEREM

Koti langu ninavua, ili nipate kunena,
Mwili wangu unaloa, japo mie sijanona,
Ulimi wanichochea, nina neno kwa vijana,
Mihadarati na pombe, vina madhara mabaya.

Si vijana si mababu, wengi wavuta sigara,
Wamesahau wajibu, pombe yawateka nyara,
Kama vile uraibu, na mengineyo mathara,
Mihadarati na pombe, vina madhara mabaya.

Vijana wengi wadogo, wamekuwa vibogoyo,
Huangukia magogo, nako kuumizwa kwayo,
Pombe huleta mapigo, kwa wale waikunywayo,
Mihadarati na pombe, vina madhara mabaya.

Mtu akilewa sana, yeye hujiita dume,
Kumbe ni dume kwa jina, hana nguvu za kiume,
Na mke wamekosana, amekuwa gumegume,
Mihadarati na pombe, vina madhara mabaya.

Walevi hujiambia, ulevi ni uungwana,
Na hali wakosa njia, watetereka mchana,
Mitaro hutumbukia, na uchafu hukumbana,
Mihadarati na pombe, vina madhara mabaya.

Ya nyumbani majukumu, wametupilia mbali,
Wanapopigiwa simu, waanza kuwa wakali,
Vinywani watema sumu, watusi bila kujali,
Mihadarati na pombe, vina madhara mabaya.

Masikini matajiri, walevi wanafanana,
Hurauka alfajiri,wazee hata vijana,
Hawana mambo ya siri, kila kitu ni bayana,
Mihadarati na pombe, vina madhara mabaya.

Wa kutetereka mwendo, huku na kule njiani,
Huanguka kwa vishindo, na kujipata ardhini,
Ile ya maji mikondo, wazuia mitaroni,
Mihadarati na pombe, vina madhara mabaya.

Ulevi hukimbilia, peupe bila kujali,
Pombe wanaibugia, tena ile kalikali,
Magari wanaingia, husababisha ajali,
Mihadarati na pombe, vina madhara mabaya.

Malenga Kulei Serem

You can share this post!

WATOTO: Subira yake katika uigizaji yamvutia heri KBC

JAMVI: Vinara watatu wa Nasa wataziba pengo la...

adminleo