Taratibu muhimu za kilimo cha mahindi
Na SAMMY WAWERU
MAHINDI pamoja na mchele, ngano, na ndizi ndiyo mazao manne yanayoliwa kwa wingi duniani.
Ngano, mahindi na mchele, yote yanaorodheshwa katika familia ya nafaka.
Ukanda wa Afrika Mashariki na hasa nchini Kenya, mahindi hutumika katika mapishi ya kande au pure, maarufu kama githeri, mlo unaopikwa kwa kuchanganya mahindi, maharagwe au punje za kunde.
Mahindi yanaposagwa, unga wake hutumika kusonga sima na hata kupika uji.
Hapa nchini, kaunti za Uasin Gishu, Trans Nzoia, Bungoma, na Nakuru ndizo zinaongoza katika uzalishaji wa mahindi.
Eneo la Kati huyakuza kwa uchache, na misimu kadhaa kwa mwaka kwa kuwa wengi hutumia mfumo wa unyunyiziaji mashamba maji kwa mifereji.
Mahindi yanaorodheshwa kwa mujibu wa muda wake kukomaa.
Kuna ya muda mfupi, kati ya siku 120 – 150, sawa na miezi minne baada ya upanzi.
Yanafahamika kwa jina maarufu kama ‘Katumani’, yakifanya vyema maeneo yaliyo mita 1600 mwinuko wa ufuo wa bahari. Wataalamu wanasema yanahitaji kiwango cha mvua milimita 800 kwa mwaka.
Yale ya muda mrefu, hasa yanayokuzwa North Rift hupandwa Machi hadi Aprili, na huanza kukomaa Septemba na Novemba.
Kwa kuwa eneo hilo huyapanda kwenye mashamba makubwa, huyaruhusu kukaukia shambani.
Huyakata na kuyakusanya kwa makundi almaarufu ‘stakes’ ambapo matawi (mihindi) yenye mahindi hutazamishwa juu.
Hupewa muda wa mwezi na wiki kadhaa, kisha yanavunwa.
Ingawa, ukuaji na uvumbuzi wa teknolojia umerahisisha shughuli za kuyavuna kupitia mashine, haswa mataifa yaliyoimarika. Kuna mashine ya aina yake, inayoendeshwa na mota ya trekta kuyadondoa punje.
Wataalamu wanahoji mahindi yanastawi maeneo yenye kiwango cha joto kati ya 18 – 27, kipimo cha nyuzijoto mchana na karibu nyuzijoto 14 usiku.
Aghalabu kiwango cha mvua inayohitajika ni milimita 1200 – 2500 kwa mwaka. Bw James Kimemia, mtaalamu hata hivyo anasema maeneo yanayopokea kimo cha milimita 600 – 1150 yanafanikisha ukuzaji wa mahindi.
“Mahindi kama vile Katumani, yanastawi maeneo yanayopata kipimo cha milimita 400, ya mvua,” Kimemia anasema.
Udongo unapaswa kuwa wenye rutuba na usiotuamisha maji.
Ule wa tifutifu ndiyo bora zaidi katika kilimo cha nafaka hii, ukipendekezwa kuwa na uchachu, pH kati ya 5.5 – 7.0. Ni muhimu maeneo lengwa, yawe kati ya mita 100 – 2900, mwinuko wa ufuo wa bahari (altitude).
Katika mashamba makubwa, hulimwa kwa trekta, halafu shamba linapewa muda wa wiki kadhaa au miezi makwekwe kukauka. Hutandazwa (harrowing) kwa mashine yenye vijisahani vikubwa, ambavyo pia hufanya udongo kuwa mwororo.
Kuna mashine za kisasa zinazotumika kupanda punje-mbegu za mahindi, pia yenye mahala pa fatalaiza, na kuzifunika kwa udongo. Wakati wa shughuli hiyo, fatalaiza aina ya DAP ndiyo bora zaidi.
Kulingana na mtaalamu James Kimemia, mashimo kwa maana ya maakoongo yanapaswa kukatwa na kuwa karibu sentimita 30 kutoka moja hadi lingine.
“Kitaalamu, nafasi ya mistari ya mashimo iwe na kati ya sentimita 75 hadi 90. Mbegu ipandwe sentimita nne kuenda chini,” anafafanua mdau huyo.
Utumizi wa mboleahai unatiliwa mkazo, na kwamba inapaswa kuwekwa kwenye mashimo kabla ya upanzi.
Vigezo muhimu katika uzalishaji wa mahindi ni maji ya kutosha, palizi na kuyastawisha kwa mbolea, haswa yenye ukwasi wa Calcium, Ammonium na Nitrogen.
Vilevile, matawi yanayojitokeza kandokando mwa mihindi yanapaswa kupogolewa.