• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
KCPE: Azoa alama 401 licha ya kumuuguza mamaye miaka 4

KCPE: Azoa alama 401 licha ya kumuuguza mamaye miaka 4

ERICK MATARA NA RICHARD MAOSI

KWA miaka minne Sharon Wangeci mwenye umri wa miaka 13 alilazimika kugawanya muda wake, kusoma na kumshughulikia mamaye mzazi aliyekuwa akiugua kansa. 

Wangeci alikuwa katika Darasa la Nne, mamake Jenniffer Wothaya alipomfichulia habari za kushtua kwamba alikuwa akiugua saratani ya matiti.

“Ilianza kama kipele kidogo lakini hali hiyo iliendelea kuwa mbaya hadi ilipofikia mwaka wa 2015,” Bi Wothaya alieleza Taifa Leo Dijitali katika mazungumzo mjini Nakuru.

Jenniffer anasema aliathirika na saratani akiwa na umri wa miaka 32 mnamo 2012, hadi sasa ambapo ana miaka 40.

Kulingana naye, haikuwa rahisi kujikubali mbali na kujumuika na wenzake katika vikao vya umma kutokana na unyanyapaa unaotokana na maradhi ya kansa. Muda mwingi alijifungia ndani ya chumba.

Wakati huo alikuwa akihudumu kama muuguzi katika hospitali moja mjini Nakuru. “Mambo hayakuwa rahisi kwa sababu hali yangu ilimsumbua binti yangu, jamaa na marafiki kimawazo, ikabidi niache kazi na kulazwa hospitalini hasa nilipoadhirika katika uti wa mgongo,” akasema.

Wakati huo binti yake alikuwa katika shule ya msingi ya Lions Nakuru, lakini licha ya maumivu hayo Wangeci alikuwa karibu na mama yake kuliko mtu yeyote yule.

“Wakati mwingi alikuwa akinitembelea hospitalini na kukosa kuhudhuria masomo yake, Wangeci alikuwa akishinda nami katika hospitali wakati mwingine kutwa nzima,” Bi Wothaya akasema.

Licha ya pandashuka nyingi familia ya Wangeci inasherehekea matokeo mazuri katika mtihani wa kitaifa wa Kenya Certificate of Primary Education (KCPE) 2019, yalipotangazwa wiki iliyopita.

Alikalia mtihani wake katika shule ya msingi ya Tenrey kaunti ya Embu na kuzoa jumla ya alama 401, akiwa miongoni mwa wanafunzi saba waliopata zaidi ya alama 400.

Mwaka wa 2018 Wothaya alifanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo nchini India, ambapo alilazwa kwa takriban miezi minane akipokea matibabu.

Hata hivyo Wangeci anasema maradhi ya mamake hayakuzima matumaini yake kufanikiwa maishani, hususan kufanya vyema katika masomo yake, ambapo analenga kuwa rubani siku za usoni.

Mamake aliporejea kutoka nchini India Wangeci alichukua jukumu la kumwangalia mamake na kwa wakati huo akiyahudhuria masomo yake , bila kupoteza dira.Wakati huo wote alimakinika masomoni.

“Ninampenda mamangu kwa sababu amenilea tangu nilipokuwa mtoto mdogo ,sisi hulala na kupiga dua pamoja kila siku na tumeunda mshikamano usioweza kuvunjika,”Wangeci alisimulia.

Kulingana na Bi Wothaya binti yake alipitia wakati mgumu wakati alipokuwa akipitia matibabu ndani na nje ya nchi, ambapo mnamo 2016 alielezwa alikuwa na miaka mitatu pekee ya kuishi lakini alisema alitamani kufa akiwa kiumbe tofauti.

Wangeci alisema alitarajia kufanya vyema katika mtihani wake wa darasa la nane na anawashaukuru walimu na wanafunzi wenzake kwa kutia moyo, na kumhimiza asikate tamaa.

Wangeci analenga kujiunga na shule ya upili ya Mary Hill Thika , huku mamake ambaye aliepuka makali ya kansa akiendelea kuwafaa watu wengine wasiokuwa na uwezo katika jamii.

Aliacha kazi ya utabibu na sasa yeye ni mchungaji huku akiwa amesimamia miradi ya Umoja wa kimataifa (UN) na USAID Afya Uzazi Scheme katika kaunti ya Nakuru na Baringo.

You can share this post!

Gereza la Shimo la Tewa lamtaka mahabusu Sonko

BI TAIFA NOVEMBA 03, 2019

adminleo