• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Canada yaitaka Kenya itoe sababu ya kumfurusha Miguna tena

Canada yaitaka Kenya itoe sababu ya kumfurusha Miguna tena

Na MWANDISHI WETU

SERIKALI ya Canada imeitaka Kenya kuwasilisha maelezo kirasmi kwa nini wakili Miguna Miguna alitimuliwa nchini kwa mara ya pili.

Hatua hiyo imefuatia madai ya Dkt Miguna kuwa alidungwa dawa na kuwekwa kwa ndege ya Emirates kuelekea Dubai , ambapo ndiyo aliweza kusafiri kuelekea Toronto, Canada.

Katika barua hiyo iliyoandikwa Machi 29 kwa ubalozi wa Kenya, Ottawa, Wizara ya Mashauri ya Kigeni, Biashara na Maendeleo Canada, inasema kuwa maelezo ya pekee iliyonayo kuhusiana na kutimuliwa kwake Dkt Miguna ni kutoka kwa vyombo vya habari na madai ya Dkt Miguna kuwa aliteswa, waliomshughulikia walitumia nguvu nyingi na kwamba alidungwa dawa ya kumlaza isiyojulikana bila idhini yake.

“Serikali ya Canada inapatia uzito madai ya kuteswa kwa raia wa Canada. Wizara inataka ubalozi kutoa maelezo rasmi kuhusiana na kutimuliwa kwake Dkt Miguna kutoka Kenya,” barua hiyo inaeleza.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni nchini, Monica Juma na Waziri Msaidizi Ababu Namwamba hawakujibu maswali yetu kubaini ikiwa ubalozi wa Kenya Ottawa umetoa maelezo hayo, na athari za suala la Miguna katika masuala ya kidiplomasia baina ya Kenya na Canada.

Mnamo Aprili 3, Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i aliambia Kamati ya Usalama ya Bunge la Kitaifa kuwa hajui ikiwa Dkt Miguna alidungwa dawa kabla ya kusafirishwa Dubai. Pia alisema kuwa wakili huyo aliondolewa kutoka upande wa ndege wa JKIA, na hakutimuliwa kama inavyosemekana.

Bw Miguna alitimuliwa nchini usiku wa Machi 28 baada ya siku tatu za mivutano kuwa aruhusiwe kuingia nchini kwa kutumia kitambulisho chake.

Hiyo ilikuwa mara ya pili ya wakili huyo ambaye alishuhudia “kuapishwa” kwa Kiongozi wa NASA Raila Odinga kama rais wa wananchi, Uhuru Park, Januari 30.

Kukamatwa na kutimuliwa kwake ni moja wapo ya misako iliyopangwa na polisi kuwakamata waliohusika na kupanga hafla hiyo ya kumuapisha Bw Odinga Uhuru Park.

Wanahabari pia waliumizwa katika harakati za kufuatia masaibu yake wakili huyo akiwa katika uwanja wa ndege wa JKIA.

 

You can share this post!

Msomi Mkenya apewa miezi 3 kuondoka Amerika

Raila hawezi kuaminika kisiasa – Gavana Waititu

adminleo