• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 2:18 PM
Pendekezo Nakuru iwe jiji kujadiliwa na Seneti

Pendekezo Nakuru iwe jiji kujadiliwa na Seneti

Na IBRAHIM ORUKO

MJI wa Nakuru huenda ukawa jiji la nne nchini ikiwa maseneta wataidhinisha pendekezo la serikali ya kaunti kutaka upandishwe hadhi kuwa jiji.

Katika ripoti yake kwa Seneti, Gavana Lee Kinyanjui alisema kuwa mji wa Nakuru umetimiza vigezo vyote vya kuuwezesha kupandishwa hadhi na kuwa jiji.

Gavana Kinyanjui alimwandikia barua Karani wa Seneti Jeremiah Nyegenye, akisema kuwa ripoti ya tume maalumu ya kutaka Nakuru kuwa jiji iliidhinishwa na Bunge la Kaunti.

Spika wa Bunge Kenneth Lusaka aliwasilisha ombi hilo mbele ya Seneti Alhamisi na akawataka maseneta kuchukulia suala hilo kwa uzito kwani lilikuwa mara ya kwanza kupokea ombi la kutaka mji upandisha kuwa jiji.

Bw Lusaka aliagiza Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi na Uhusiano wa Serikali kuwasilisha ripoti yake kuhusiana na ombi hilo Februari mwaka ujao.

“Hii ni mara ya kwanza kupokea ombi la aina hii. Maseneta wanafaa kuchukulia suala hili kwa uzito na kamati husika iwasilishe ripoti itakayojadiliwa mwaka ujao,” akasema Bw Lusaka.

Kifungu cha 7 cha Sheria ya Miji na Majiji kinasema kuwa: “Rais, kwa kuzingatia mapendekezo ya Seneti, anaweza kupandisha hadhi ya mji wa manispaa kuwa jiji.”Ikiwa Rais Kenyatta atapandisha hadhi mji huo, Nakuru litakuwa jiji la nne baada ya Nairobi, Mombasa na Kisumu.

Sheria ya Miji na Majiji inahitaji kuwa mji unopewa hadhi ya jiji uwe na wakazi zaidi ya 500,000 na uwe na uwezo wa kuzalisha mapato ya kuendesha shughuli zake.

Mahitaji mengineyo ni miundomsingi kama vile taa, barabara, masoko, vituo vya zimamoto na utaratibu mwafaka wa kukusanya na kutupa takataka.

You can share this post!

Waliomuua mwanahabari wa The Star kushtakiwa

Maafa zaidi

adminleo