TAHARIRI: Jisomee ripoti ya BBI mwenyewe uielewe

NA MHARIRI

RIPOTI ya Jopo lililoundwa kukusanya maoni ya wananchi kuhusu njia ya kuleta maridhiano nchini inasubiriwa kwa hamu kuu inapotarajiwa kutangazwa Jumatano.

Itakapokabidhiwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, ripoti hiyo itamaliza dukuduku ambalo Wakenya wamekuwa nalo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Lakini pia kutolewa kwa ripoti kutafungua ukurasa mpya, wa kuwapa nafasi wananchi kuisoma na kuijadili kwa kina, kabla ya kutoa maoni yao kuihusu.

Ripoti hiyo, kama alivyogusia mmoja wa makatibu wa jopo la BBI, wakili Paul Mwangi, imegusia karibu kila jambo linalohusiana na utangamanao, uchumi na hali ya maisha ya baadaye ya nchi hii kwa jumla.

Kupitia ripoti hii, inatarajiwa kuwa Wakenya wakiridhika nayo, watapendekeza marekebisho ya kufanywa kwenye katiba yetu, ambayo sasa imetimiza zaidi ya miaka tisa.

Marekebisho hayo kawaida hapa nchini yamekuwa yakiandamana na siasa kali, za wanaopinga na wanaokubali. Hata sasa hivi, hali haitakuwa tofauti.

Tayari wanasiasa wameonyesha kutoa hisia kinzani hata kabla hawajaiona. Kwa hivyo, haitakuwa ajabu iwapo kutazuka upande utakaokataa na utakaounga mkono mapendekezo hayo. Na hiyo ndiyo demokrasia.

Hata hivyo, katika malumbano hayo, wananchi wanapaswa kutumia busara na kujisomea ripoti hiyo kwa makini, ili wapambanue ukweli na uongo kutoka kwa wanasiasa watakapokuwa majukwaani.

Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya Wakenya wanajua kusoma na kuandika.

Kutolewa kwa ripoti hii yafaa kuwape nafasi ya kusoma kwa kila kila kipengee, badala ya kusikiza propaganda zitakazoenezwa kwa kila njia, ikiwemo mitandao ya kijamii.

Wakati wa kampeni za ‘Ndizi’ na ‘Chungwa’ wanasiasa waliokubali na waliopinga waliwashawishi wafuasi wao kuwa pande zao, bila ya kuwapa nafasi ya kuelewa walichokuwa wapinga au kuunga mkono.

Kuna wakati wafuasi wa Bw Odinga walisikika wakisema kuwa maadamu ‘Baba amesoma’ kila kitu kiko shwari.

Huu ni mtazamo usiofaa kwa watu wanaotarajiwa kupata nchi bora kwao na kwa vizazi vyao.

Ikiwa tunataka kuwa na nchi nzuri, ni lazima kila mtu ajisomee na kuchagua kilicho bora bila ya kushinikiwa na wanasiasa.

Habari zinazohusiana na hii

Refarenda yaja