• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
BBI: Ubaguzi umekolea katika kaunti

BBI: Ubaguzi umekolea katika kaunti

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA wanasema serikali za kaunti zimejawa na ubaguzi wakati wa uajiri, ugavi wa rasilmali na huduma huku wanasiasa wakiingilia bodi za huduma za kaunti na kunyima baadhi ya maeneo miradi ya maendeleo, inaeleza ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI).

Ingawa katiba ya 2010 ilibuni ugatuzi kwa lengo la kupeleka mamlaka mashinani na kuimarisha huduma kote nchini, Wakenya waliambia jopokazi hilo kuwa magavana na wanasiasa wamekuwa wakibagua baadhi ya wadi na jamii katika kaunti zao.

“Wakenya wanataka wahusishwe zaidi katika utoaji wa huduma na miradi ya maendeleo ili kuepuka pesa kutumiwa vibaya na ufisadi,” inaeleza ripoti ya BBI iliyotolewa kwa umma jana.

Inasema kuwa Wakenya wanahisi wametengwa na serikali katika maamuzi yanayohusu kaunti zao.

“Kuwachukulia Wakenya kana kwamba hawana haki na nguvu katika sera, sheria, bajeti na miradi ya maendeleo ni jambo la kawaida katika serikali za kaunti. Kaunti zimejawa na ufisadi, ubaguzi na miradi ya maendeleo isiyoafiki mahitaji ya maeneo yao na isiyotekelezwa vyema,” inaeleza ripoti hiyo.

Inaeleza kuwa ilivyo katika serikali ya kitaifa, serikali za kaunti zinatumia gharama kubwa kulipa mishahara, zimekolewa na ubaguzi na siasa za mgawanyiko na ukosefu wa maadili.

Ripoti inapendekeza kuwa bodi za huduma za kaunti ziwe huru na zipewe majukumu ya kuajiri wafanyakazi, kuweka viwango vya mishahara vinavyotoshana na vya serikali ya kitaifa na kutimiza ushirikishi.

Kote nchini, Wakenya walilia kwamba seikali na mabunge ya kaunti yamekolewa na ufisadi ambao unalemaza maendeleo huku maslahi ya kisiasa yakitawala.

“Viongozi wa maeneo pia walilaumiwa kwa kupuuza sheria wakilenga kutimiza maslahi ya kibinafsi. Ikiwa ufisadi katika kaunti hautakomeshwa, utaporomosha ugatuzi,” inaeleza ripoti hiyo.

Ingawa inapendekeza kaunti 47 zidumishwe, ripoti inasema zimeshindwa kukusanya mapato ya kutosha na hata kueleza zinavyotumia zinazokusanya. Ripoti inapendekeza mgao wa pesa kwa kaunti ulenge zaidi sekta za kilimo, afya na ustawi wa miji.

Aidha, inapendekeza majukumu yote yanayotolewa na mashirika ya serikali katika serikali za kaunti yasitishwe na kuwianishwa na ugatuzi.

“Mfumo wa ugavi wa mapato unapaswa kuwa rahisi ili raia wauelewe,” inaeleza ripoti hiyo.

Ripoti inapendekeza madiwani wasimamie pesa zinazotengewa basari. Inasema maeneo ambayo yamekuwa yametengwa kwa miaka mingi yanapaswa kupigwa jeki kupitia hazina ya usawazishaji lakini iwe kwa muda utakaowekwa.

Ripoti inapendekeza kuwa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) inapaswa kuchunguza kiwango cha pesa kila kaunti inachokusanya na kukishirikisha katika mgao wa kila mwaka.

Ili kuzuia ubaguzi, ripoti inapendekeza kila wadi itengewe asilimia 30 ya pesa za maendeleo katika bajeti ya kaunti katika kipindi cha miaka mitano.

Ripoti inapendekeza kuwe na kiwango cha wafanyakazi ambao kila kaunti inafaa kuajiri kwa kutengemea idadi ya watu na idadi ya wizara ambazo kila gavana anafaa kubuni.

Ikitekelezwa, Mdhibiti wa Bajeti anatakuwa akikagua na kuthibitisha pesa zinazotengewa miradi ya kaunti zitatumiwa vyema kabla ya serikali za kaunti kupatiwa pesa zaidi.

You can share this post!

BBI: Wadhifa wa Kiongozi Rasmi wa Upinzani kurudishwa

Mtihani wa KCSE 2019 wafika tamati

adminleo