• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 7:25 PM
BBI: Hatutakaa kimya mkihatarisha Afrika Mashariki, Magufuli aonya Kenya

BBI: Hatutakaa kimya mkihatarisha Afrika Mashariki, Magufuli aonya Kenya

Na MARY WANGARI

RAIS wa Tanzania John Pombe Magufuli amewatahadharisha viongozi wakuu Kenya akiwemo Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga dhidi ya kuchochea vurugu nchini zinazoweza kuathiri Eneo la Afrika Mashariki.

Bw Magufuli aliyewakilishwa na mjumbe wake Profesa Palamagamba Kabudi katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya jopokazi la Building Bridges Initiative (BBI) iliyoandaliwa jana Bomas of Kenya, Nairobi, alisema kuwa hafla hiyo haikuwa tu ya kitaifa bali ilihusu eneo lote la Afrika Mashariki.

“Rais Magufuli anasema nyinyi watatu ni vizingiti muhimu vya Kenya. Rais Uhuru wewe ni Mtanzania tafadhali dumisha heshima ya Tanzania, mheshimiwa Raila Kenya ni muhimu zaidi yako, mheshimiwa Ruto, Mungu aliyekupa wadhifa huo ndiye atakayekupa uwezo wa kuinusuru Kenya,’

“Umoja kitaifa unapaswa kuwa ajenda yenu ya kwanza wakati wa kutekeleza BBI. Hatutaingilia masuala yenu ya nchi lakini tukiona mkifanya mambo yanayohatarisha eneo la Afrika Mashariki hatutachelea kuzungumza,’ alitahadharisha mjumbe huyo maalum kutoka Tanzania.

Aidha, Bw Kabudi aliwahimiza wanasiasa kujitenga na siasa za kikabila na kutimiza matarajio ya Wakenya kwa kutilia maanani maslahi ya raia nchini na eneo la Afrika Mashariki kwa jumla.

Huku akimpongeza Bw Uhuru kwa hatua hiyo, Bw Magufuli kupitia mjumbe wake aliahidi kuunga mkono Kenya kuhusu wadhifa wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Uhuru alisimulia jinsi hali ilivyokuwa wakati wa kikao maalum na kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) saa chache kabla ya handisheki maarufu ya 2018.

“Kukutana kwetu mara ya kwanza haikuwa rahisi. Tulikuwa na hofu sawa na wananchi kote nchini. Tulikunywa chai pamoja kwa dakika kama 45 bila kusema lolote kwa kuwa hatukujua la kusema.

“Tuliishia kuulizana, ‘mama yuko salama?’ Ndio yuko salama’, Vipi kuhusu watoto, wako salama, wanasoma,” alikumbuka rais Uhuru huku umati ukiangua kicheko.

Bw Uhuru alieleza kwamba ni baada ya kujadiliana na kuona kuwa tofauti kati yake na Bw Raila zilikuwa ndogo ikilinganishwa na kiwango cha mashindano kati yao.

“Tulijiuliza ni kwa nini kila baada ya uchaguzi ni sharti kuzuke vurugu? Tunataka mfumo ambapo kila Mkenya atajihisi kuwa mshindi, ambapo atatulia akijua yeyote atakayeibuka mshindi hatampokonya shamba wala kumnyima kazi,” alisema rais akiwahimiza viongozi kutilia maanani mambo yanayoweza kuwaunganisha Wakenya kinyume na kuangazia tofauti zao.

Hata hivyo, nusura hafla hiyo ivurugike Kiongozi wa Wengi na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, aliposimama kuzungumza na kuamua kufungua moyo kuhusu unafiki wa baadhi ya wanasiasa katika hafla hiyo.

Licha ya halaiki ya watu wengi wao kutoka mrengo wa Kieleweke kujaribu kumnyamazisha, seneta huyo mkakamavu anayeegemea mrengo wa TangaTanga alisimama kijasiri huku akisema ni sharti mfumo wa siasa urekebishwe ili kumpa kila mtu fursa ya kusikika bila kujali anakotoka.

“Tunaanza kusafisha siasa wetu. Kila mwananchi ni sharti apate nafasi ya kueleza hisia zake hata huyo Mrendile ambaye huenda hatapata fursa ya kuwa rais ama waziri mkuu. Tunataka taifa ambalo hali ya kubaguliwa kwa misingi ya kilkabila itakuwa jambo la jadi,” alisema Bw Murkomen.

You can share this post!

BBI: Wanasiasa watatimiza ahadi hizi?

BBI: Ruto na Mudavadi waonya kuhusu kugawa mamlaka

adminleo