• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
BBI: Ruto na Mudavadi waonya kuhusu kugawa mamlaka

BBI: Ruto na Mudavadi waonya kuhusu kugawa mamlaka

Na JUMA NAMLOLA

NAIBU Rais William Ruto na kinara wa chama cha Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi wamewakosoa wanasiasa ambao wameanza kupigia debe masuala ya ugawaji wa nyadhifa za kisiasa badala ya kuwa na mtazamo mpana kuhusu Ripoti ya BBI.

Akihutubu wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jana katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, Bw Mudavadi aliwakemea wanasiasa aliodai hawajali maslahi ya mwananchi.

“Niliposikiza hotuba za wenzangu waliotangulia, naona tumegeuza mjadala kuhusu ripoti ya BBI kuwa lengo lake hasa ni kusambaza mamlaka kwa wanasiasa. Mheshimiwa Rais, uchumi, uchumi, uchumi,” akasema.

Bw Mudavadi alisikitika kwamba Kenya ni miongoni mwa mataifa machache ulimwenguni ambapo maelfu ya watu hawana shughuli za kuwapatia riziki.

“Kenya ni nchi moja ya zile chache duniani ambapo ukiitisha mkutano wa kisiasa siku ya kazi, uwanja utafurika. Hii inatuonyesha nini? Kwamba tuna mamilioni ya watu wasiokuwa na ajira wala shughuli za kiuchumi,” akasema.

Ingawa hakufafanua zaidi kuhusiana na walioshinikiza kuhusu nyadhifa za kisiasa, Bw Mudavadi alionekana kujibu kauli za viongozi kadhaa, akiwemo magavana Anne Waiguru (Kirinyaga) na Charity Ngilu (Kitui) ambao walisisitiza haja ya kugawa nafasi za uongozi kati ya wanawake na wanaume.

Dkt Ruto alionya kuwa malengo ya kuundwa kwa jopo la Maridhiano hayatatimia, iwapo ugawaji mamlaka miongoni mwa wanasiasa utatawala mjadala wa kitaifa.

“Lazima tuwe waangalifu kuwa shughuli hii haitekwi nnyara na wanasiasa na kuanza kuzungumza kuhusu jinsi ya kugawa mamlaka. Ni lazima tuhakikishe kuwa tunaangazia matakwa ya Wakenya,” akasema.

You can share this post!

BBI: Hatutakaa kimya mkihatarisha Afrika Mashariki,...

BBI: Murkomen alivyojaribu kuvuruga hafla

adminleo