• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 4:28 PM
BBI: Murkomen alivyojaribu kuvuruga hafla

BBI: Murkomen alivyojaribu kuvuruga hafla

Na MARY WANGARI

MBWEMBWE, vifijo, nderemo na vigelegele ndiyo mandhari yaliyopamba sherehe za uzinduzi rasmi wa ripoti ya Buiding Bridges Initiative (BBI) iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na kuhudhuriwa na wanasiasa kutoka vyama mbalimbali nchini na wajumbe maarufu kimataifa.

Hafla hiyo ambayo bila shaka ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu ilianza kwa kisanga awali asubuhi huku baadhi ya wananchi wakiparamia kupata nafasi katika ukumbi mkuu ili kuweza kufuatilia vyema matukio.

Kinyume na hafla nyinginezo za umma, maafisa wakuu serikalini wakiwemo mawaziri, magavana maseneta, wabunge, wanasiasa na viongozi wa zamani walikuwa miongoni waliowasili katika hafla hiyo ya kihistoria nchini.

Walifuatiwa na Kiongozi wa Orange Democratic Movement Raila odinga, Naibu Rais Dkt William Ruto na Rais Uhuru Kenyatta, waliowasili kwa kishindo mtawalia katika Bomas, mtaani Karen.

Kinyume na viongozi wengine waliojikwatua vilivyo kwa suti na tai zilizonyoroshwa kwa pasi, Kiongozi wa Taifa, kama kawaida yake, aligeuka kivutio alipojitokeza kwa mavazi ya aina yake, yaliyosawiri utamaduni wa Kiafrika.

Kana kwamba alikuwa akifuata amri yake binafsi aliyotoa mnamo Alhamisi, Oktoba 17, kwa maafisa wa umma kuvalia mavazi ya Kiafrika, rais Uhuru alijitokeza akiwa amevalia shati aina ya Ankara lililokuwa na mchanganyiko wa rangi ya kijivu, nyeupe na hudhurungi na kuiambatisha na suruali ndefu nyeusi.

Wakati wa hotuba uliwadia huku viongozi walioratibiwa kuzungumza wakiitwa mmoja baada ya mwingine kuambatana na hadhi yao katika hafla hiyo.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Francis Atwoli aliivunja mbavu hadhira alipoanza kwa mtindo wake wa kawaida kwa sauti nzito iliyowagutusha watu.

“Naam, naam. Ahsante sana mheshimiwa Rais wa Kenya na wageni wote walioalikwa, alinguruma huku umati ulioshtuka ukiangua kicheko.

Hata hivyo, hali iligeuka kuwa sintofahamu wakati Kiongozi wa Wengi katika Seneti na Seneta wa Elgeyo Marakwet, aliposimama na kuamua kufungua moyo wake kuhusu unafiki miongoni mwa wanasiasa katika hafla hiyo.

Seneta huyo anayeegemea mrengo wa Tanga Tanga alijipata mashakani na kumlazimu mwenyekiti wa jopokazi la BBI Bw Mohamed Yusuf Haji kuingilia kati kujaribu kutuliza hali, baada ya halaiki ya watu wengi wao wanaounga mkono mrengo wa Kieleweke, kutaka kumnnyamazisha na kumzuia kutoa hotuba yake.

Hata hivyo, wakili huyo jasiri anayefahamika kwa ukakamavu wake na kutochelea kuelezea hisia zake, alisimama kidete na kuendelea na aliyotaka kusema.

“Tunaanza kusafisha siasa zetu. Kila Mkenya ni sharti apate fursa ya kusikika hata awe Mrendile ambaye huenda asiwe rais au waziri mkuu. Tunataka taifa ambalo kila mtu ataweza kujieleza na suala la ubaguzi wa kikabila litazikwa katika kaburi la sahau,” alisema Bw Murkomen kwa ujasiri.

You can share this post!

BBI: Ruto na Mudavadi waonya kuhusu kugawa mamlaka

BBI: Lengo ni kuzuia vita kila baada ya uchaguzi

adminleo