Michezo

Ripoti ya BBI inavyosema kuhusu kusuka talanta za vijana chipukizi

November 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN ASHIHUNDU

RIPOTI ya Jopo la Maridhiano (BBI) imependekeza kubuniwa kwa taasisi ya kitaifa ya kusimamia michezo ya bahati nasibu, kama ilivyo katika mataifa yaliyoendelea, huku mapato yake yakikusudiwa kuinua maisha ya vijana kupitia miradi ya kuboresha michezo, utamaduni na masuala mengine ya kijamii.

Katika ripoti iliyozinduliwa rasmi Jumatano kwenye ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, BBI inapendekeza kupigwa marufuku kwa kampuni zote za bahati nasibu, kwa madai kwamba zimeharibu maisha ya vijana wengi ambao wamekuwa maskini baada ya kushiriki katika shughuli za kamari.

Kabla ya ripoti hiyo kutolewa, tayari Serikali ilikuwa imeongeza ushuru inaotoza kampuni za kamari kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 35 ya mapato yao.

Ushuru huo wa juu unanuia kuzuia watoto na vijana wadogo kutekwa na uraibu wa kubashiri matokeo ya michezo, ambao ulikuwa umemeza Wakenya wengi hususan walio na miaka kati ya 17 na 35.

Wakenya wengi hutumia simu za rununu kubashiri matokeo ya ligi za nyumbani na zile za nje, hasa Ulaya.

Wazazi na viongozi wa kidini walikuwa mstari wa mbele kuomba serikali kuchukua hatua. Bunge awali lilipendekeza ushuru wa asilimia 50 lakini Rais akaipunguza hadi asilimia 35.

Hatua hiyo, hata hivyo, ilifanya kampuni za kamari kufungwa hususan SportPesa na Betin zilizokuwa zikidhamini michezo ya soka, raga na ndondi.

Mashirikisho mbalimbali ya michezo ikiwemo Kampuni ya Kenya Premier League inayosimamia timu za Ligi Kuu ya Kenya (KPL), sawa na klabu za soka za Gor Mahia na AFC Leopards, ni miongoni mwa zilizoathirika pakubwa.

Kenya iko na taasisi moja ya kitaifa inayoendesha kamari kwa jina Kenya Charity Sweepstake, iliyoanzishwa 1962. Lakini sio maarufu kama zilivyo zinginezo katika mataifa yaliyoendelea.

Hisa

Majuzi, kampuni ya kigeni ya Tenlop Group Ltd ya Uingereza, ambayo ni kitengo cha kampuni ya Elenilto Group Ltd, ilikubaliwa kuchukua asilimia 85 ya hisa za Kenya Sweepstake.

BBI inapendekeza pesa zitakazokusanywa na taasisi ya kitaifa ya kamari, zitumike kusaidia vijana mashinani kukuza talanta zao za spoti na pia biasahara.

Kadhalika ripoti hiyo inaitaka serikali kuweka mikakati ya kina kuratibu, kufadhili na kukuza sanaa na spoti, miongoni mwa fani mbalimbali ambazo vijana wa Kenya wanadhihirisha talanta vipaji vyao.

Hata hivyo, ripoti hiyo ya BBI haikuzungumzia chochote kuhusu Hazina ya Spoti ambayo ndiyo inatekeleza wajibu huo wa taasisa ya kitaifa ya kamari.