Habari

Balozi wa Amerika nchini Kenya asema BBI inaleta matumaini

November 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

BALOZI wa Amerika Kyle McCarter Alhamisi aliongoza sherehe ya maadhimisho ya Sikukuu ya Kutoa Shukrani aliposhiriki mlo wa mnofu wa batamzinga pamoja na wahariri na waandishi wa habari wa shirika la habari la Nation (NMG) katika jumba la Nation Centre, Nairobi.

Hii ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa balozi wa Amerika kuadhimisha sikukuu hiyo pamoja na wanahabari wa NMG.

Sikukuu hiyo husherehekewa kila mwaka mwezi Novemba nchini Amerika ambapo wananchi hutoa shukrani kwa Mungu kwa ufanisi ambao amewawezesha kufikia.

Balozi wa Amerika nchini Kenya, Kyle McCarter akata mnofu Novemba 28, 2019, jijini Nairobi. Picha/ Charles Wasonga

“Hii ni siku muhimu zaidi nchini Amerika na ambayo huadhimishwa Alhamisi ya mwisho wa Novemba kila mwaka. Waamerika hutumia siku hii kutoa shukrani kwa Maulana kwa mafanikio katika nyanja zote za maisha, hasa uchumi. Hii ndiyo maana ninashirikiana nanyi Wakenya kama marafiki wetu kuadhiminisha siku hii,” akasema Bw McCarter.

Kuhusu ripoti ya jopo la maridhiano (BBI), balozi huyo alisema imesheheni mapendekezo mazuri ambayo yatasaidia kuwaunganisha Wakenya.

“Amerika iko tayari kusaidia mpango wowote unaolenga kuleta umoja na maendeleo katika taifa hili. Na hii ndiyo maana tunaunga mkono mapendekezo ya ripoti ya BBI na kuwaonya wanasiasa dhidi ya kuitumia ripoti kuwagawanya Wakenya,” Bw McCarter akasema.

Aliongeza kuwa Amerika inaunga mkono Kenya katika vita dhidi ya ufisadi ambao aliutaja kama uovu unaohujumu maendeleo nchini.

“Serikali ya Amerika itaendelea kuelekeza rasilimali katika asasi za kupambana na jinamizi hili ili kuimarisha utendakazi wazo. Asasi hizo ni kama vile tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) na Idara ya Mahakama,” Bw McCarter akaongeza.

Akihutubu baada ya kukata mnofu, Bw McCarter aliwahimiza Wakenya kupalilia moyo wa upendo na ushirikiano.