Habari Mseto

Maporomoko yaua wawili baada ya mvua iliyopitiliza

December 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PIUS MAUNDU Na CHARLES WASONGA

WATU wawili walifariki Jumamosi katika mkasa wa maporomoko ya ardhi katika kijiji cha Kilungu, Kaunti ya Makueni.

Kamanda wa Polisi katika kaunti hiyo, Bw Joseph ole Napeiyan alisema, watu wengine walijeruhiwa katika mkasa huo huku zaidi ya familia 20 zikiachwa bila makao.

Haya yanajiri huku Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga ikitangaza kuwa mvua kubwa itaendelea kushuhudiwa katika kaunti 19 nchini, ikiwemo Makueni, huku serikali ikitangaza mpango wa kuomba misaada kusaidia waathiriwa wa janga hilo.

Mnamo Novemba 22, zaidi ya watu 43 walifariki na wengine wengi kujeruhiwa katika mkasa wa maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya Pokot Magharibi kufuatia mvua kubwa iliyonyesha eneo hilo.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Ijumaa, idara hiyo ilisema kaunti hizo za maeneo ya South Rift, Central Rift na Nyanza yatashuhudia mvua kubwa kuanzia Novemba 29 hadi Desemba 4.

Naye Waziri wa Fedha, Bw Ukuru Yatani alisema serikali, kupitia wizara hiyo, itashirikisha misaada kutoka humu nchini na nje, kwa ajili ya kukabiliana na athari za mvua hiyo.

“Kutokana na hali hii ya dharura, kwa msingi wa mamlaka niliyopewa chini ya sheria ya usimamizi wa fedha za umma, ninatangaza mpango wa kukusanya misaada kutoka nchini na mataifa ya nje kukabiliana na janga hili,” akasema Bw Yatani katika taarifa iliyochapisha magazetini jana.

Na idara ya utabiri wa hali ya anga iliongeza kuwa kuna uwezekano wa mvua kubwa kushuhudiwa pia katika maeneo ya Kati mwa Kenya, Nairobi na maeneo ya Kusini Mashariki.

Mkurugenzi katika idara hiyo David Gikungu aliwataka Wakenya kuchukua tahadhari kuzuia maafa na uharibifu wa mali.