Habari MsetoSiasa

Wazee wa Pwani wakataa BBI

December 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA FADHILI FREDRICK

Baraza la wazee wa jamii za eneo Pwani, limepinga ripoti ya Jopokazi la maridhiano (BBI) wakidai kuwa haikutilia maanani changamoto zinazosibu wakazi wa eneo hilo.?

Mwenyekiti wa baraza hilo, Suleiman Yeya, amesema kuwa ripoti hiyo haikutoa suluhu kwa suala tata la ardhi Pwani ikiwemo dhuluma za kihistoria zilizofanyiwa wenyeji na serikali zilizopita.

‘Nimeipitia ripoti hiyo lakini haijatoa suluhu mwafaka kuhusu masaibu ya wakazi wa Pwani katika suala tata la ardhi na ndio maana tunaipinga ripoti hiyo,’ akasema.

Pia, Bw Yeya amekashifu kubuniwa kwa nafasi ya waziri mkuu, akisema rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga wanalenga kusalia madarakani.

Licha ya baraza hilo kupinga ripoti baadhi ya wakazi na viongozi Kaunti ya Kwale wameipigia upatu ripoti hiyo.

Gavana Salim Mvurya anaunga ripoti hiyo akisema imeunganisha Wakenya na mapendekezo yake yatazima uhasama na fujo zinazoshuhudiwa kila baada ya uchaguzi nchini.

Vilevile, Bw Mvurya alisema ripoti hiyo imeangazia nyongeza ya mgao wa fedha katika kaunti ili kuendeleza shughuli za kimaendeleo.

‘Tatizo kubwa linalokumba kaunti nyingi ni mgao mchache wa fedha na hiyo imekuwa changamoto kwetu kutekeleza miradi ya maendeleo lakini kupitia ripoti hii tuna matumaini ya kufanikisha ajenda za maendeleo,’ akasema.

Bw Mvurya aliongeza kwamba amefurahishwa na mapendekezo ya kuwawezesha wanawake katika nyadhifa za uongozi hususan kwenye viti vya ugavana kuwa ni sharti naibu gavana awe mwanamke.