BBI yaibua mjadala mkali Thika
Na LAWRENCE ONGARO
RIPOTI ya Jopokazi la maridhiano (BBI) imezua mjadala mkali Jumapili miongoni mwa viongozi na wananchi mjini Thika.
Mbunge wa Thika Bw Patrick ‘Jungle’ Wainaina amesema anaiunga mkono ripoti hiyo ya BBI lakini akawashauri wananchi wawe mstari wa mbele kuisoma kwa makini ili kila mmoja awe na maoni yake kamili.
‘Tungetaka kuona kila mmoja wetu akichukua jukumu la kujisomea ripoti hiyo kwa makini ili baadaye asije kupotoshwa kutoa maamuzi yasiyofaa,’ alisema Bw Wainaina.
Hata hivyo alisema licha ya kuiunga mkono lakini hakubaliani na mtindo wa kutaka kugawanya mamlaka kwa viongozi wachache.
‘Ripoti hiyo kwa hakika inaangazia maswala mengi muhimu inayoweza kunufaisha mwananchi wa kawaida lakini hata hivyo kila mmoja anastahili kutoa maoni yake bila kushinikizwa kufuata ya mwingine,’ alisema Bw Wainaina.
Aliyasema hayo Ijumaa eneo la Gatuanyaga, Thika Mashariki, wakati wa mazishi ya watoto wawili walioangamia kwa ajali ya barabara kuu ya Thika-Kenol majuzi.
Naibu Gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alisema siku ya kitamaduni ya kukumbuka BBI ni muhimu kwa nchi yetu kwa sababu inaleta utangamano miongoni mwa wananchi.
‘Huu ndio wakati wa kila mmoja kujitokeza na kujisomea ripoti hiyo ili baadaye watu wajiamulie ni jambo lipi wanalolitaka kupitia ripoti hiyo,’ alisema Dkt Nyoro.
Alitoa pendekezo siku ya Januari Mosi, litambuliwe kama siku ya kitamaduni.
Wakazi wengi wa Kiambu waliohojiwa walisema tayari wameisikia ripoti hiyo na kile kilichosalia ni kuketi chini kwa makini na kujisomea ili kutoa uamuzi unaofaa kwao.
‘Mimi nitafanya juhudi nijaribu kuisoma halafu baadaye nitatoa maoni yangu. Wakati huu sio wa kusomewa na yeyote, lakini nitajiamulia mwenyewe,’ alisema James Muturi, ambaye ni mkazi wa Thika.
Wengi wa wananchi waliohojiwa walikiri ya kwamba bado hawajaisoma ripoti hiyo kwa makini lakini wanatarajia kufanya hivyo bila kusomewa na viongozi.